1 Tukio la tetemeko:
Tarehe 10/09/2016 saa 9 na dakika 27 mchana kumetokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Kitovu
cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya latitudo 10 06’ na longitudo
31055’ eneo ambalo ni kilomita 20 kaskazini mashariki mwa kijiji cha
Nsunga na kilomita 42 kaskazini magharibi mwa mji wa Bukoba (Picha Namba
1 na 2). Kitovu hicho kilikuwa kilomita 10 chini ya ardhi kwenye eneo
hilo.
Picha Namba 2: Kitovu cha tetemeko la ardhi Kagera (Nyota nyekundu)
Nguvu
za mtetemo wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli ya
“Richter” ukubwa ambao ni wa juu sana kiasi cha kuleta madhara makubwa.
Kutokana na ukubwa huu maeneo mengi ya mkoa wa Kagera ikijumuisha mji wa
Bukoba yamepatwa na madhara makubwa sana ikijumuisha nyumba nyingi
kupasuka (Picha Namba 3 na 4), watu wengi kujeruhiwa kwa kuangukiwa na
vifusi na kuta za nyuma ambapo inakisiwa kuwa watu 13 wamepoteza maisha
yao.
Picha namba 4: Nyumba ziliyobomolewa na tetemeko la ardhi Bukoba.
2 Sababu za kutokea tetemeko hilo:
Kwa
kuwa kitovu cha tetemeko hilo kiko chini sana ya ardhi (Km 10) na kwa
kutafasiri umbile la mawimbi ya tetemeko hilo yaliyonakiliwa na vituo
vya kupimia matetemeko ya ardhi (Picka Namba 5) inaonekana kuwa tetemeko
hilo limetokana na misuguano ya mapange makubwa ya ardhi iliyopasuliwa
na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa. Kwa kuwa
eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi liko karibu na mkondo wa
magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki inakisiwa kuwa mtetemo huu
umesababishwa na kuteleza na kusiguana ka mapande ya miamba juu ya
mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.
Picha Namba 5: Umbile la mawimbi ya tetemeko la ardhi la tarehe 10 Septemba mkoani Kagera.
3 Upimaji wa matetemeko ya ardhi.
Mapaka
sasa na duniani kote hakuna vifaa au taratibu za kuweza kutabiri
utokeaji wa matetemeko ya ardhi. Vifaa vyote na taratibu zote za
kuratibu/kupima matetemeko ya ardhi vinapima ukubwa na tabia ya tetemeko
baada ya tetemeko kutokea.
4 Tafiti za kina.
Wakala
wa Jiolojia Tanzania umepeleka wataalamu katika eneo la tukio ili
kuendelea kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko hilo. Taarifa zaidi
juu ya tukio hili zitaendelea kutolewa kulingana na matokeo ya tafiti
hizo pamoja na tafasiri ya taarifa na takwimu za matetemeko ya ardhi
zinazonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi nchini hususan
kituo cha Geita ambacho ndicho kilicho karibu sana na eneo la tetemeko
hili .
5 Mambo Muhimu ya Kuzingatia Kuepuka Madhara Yanayoweza Kusababishwa na Tetemeko la Ardhi
i. Kabla ya tukio:
(a)
Elimu ya tahadhari inapaswa itolewe ili kila mmoja aelewe nini cha
kufanya linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo
kutoka kwa watu wa msalaba mwekundu kuhusu namna ya kuhudumia majeruhi
ama wahanga na pia jeshi la zima moto ili kupata elimu kuhusu namna ya
kutumia kizimamoto. Elimu na mafunzo hayo yatasaidia kuwaweka watu
katika hali ya tahadhari na hii itasaidia kupunguza taharuki wakati wa
tukio kwa vile watakuwa sasa wanajua namna ya kuchukua tahadhari.
(b)
Kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari hizo mara kwa mara ili kujizoesha
kwani mara nyingi wakati wa matukio ya majanga kama hayo watu huchelewa
kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru kwani huwa bado wanajiuliza kwamba
wafanye nini. Hivyo mazoezi ya mara kwa mara ya jinsi ya kuchukua
tahadhari humfanya mtu kufanya uamuzi wa haraka pindi tukio linapotokea.
(c)
Wananchi pia wanashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa kuzingatia
viwango halisi vya ujenzi, kuweka misingi imara wakati wa ujenzi, kupata
ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa katika eneo
husika kulingana na ardhi ya mahali hapo, kuepuka ujenzi wa nyumba
katika miinuko mikali yenye kuambatana na mawe/ miamba (suspended
boulders) na kuepuka ujenzi wa makazi katika maeneo tete yenye mipasuko
ya miamba (faults) na uwezekano mkubwa wa kutokea matetemeko.
ii Wakati wa tukio:
(a)
Wakati wa tukio la tetemeko la ardhi unashauriwa kukaa mahali salama
kama vile sehemu ya wazi isiyo na majengo marefu, miti mirefu na miinuko
mikali ya ardhi. Watu wanashauriwa kukaa nje ya nyumba katika sehemu za
uwazi.
(b)
Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa ukae chini
ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta na pia
ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha ili
kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo.
(c)
Unashauriwa usitembee umbali mrefu kwa lengo la kutafuta mahali salama
kwa sababu tetemeko la ardhi hutokea ghafla na huchukua muda mfupi.
Takwimu zinaonesha kwamba watu wanaotaharuki na kukimbia ovyo wakati wa
tukio la tetemeko ndio hupata madhara ama kuumia.
(d) Salimisha macho yako kwa kuinamisha kichwa chako wakati wa tukio.
(e)
Baki mahali salama hadi hapo mitetemo itakapo malizika na kisha
ujikague kuona kama hujaumia na ndipo utoe msaada kwa wengine ambao
watakuwa wameumia.
(f) Ondoka mahali ulipo kwa uangalifu kuepuka vitu ambavyo vitakuwa vimedondoka na kuvunjika kwani vinaweza kukudhuru.
(g)
Jiandae kwa mitetemo itakayofuata baada ya mtetemo mkuu. Tetemeko kuu
huwa mara nyingi linafuatiwa na mitetemo mingi midogo midogo.
(h)
Kumbuka kuwa matukio ya matetemeko ya ardhi huweza kuambatana na moto
hivyo jihadhari na matukio ya moto kwa vile tetemeko la ardhi linaweza
kusababisha kupasuka kwa mabomba ya gesi au kukatika kwa nyaya za umeme
ama kuharibika kwa vifaa vinavyotumia umeme na kusababisha hitilafu ya
umeme.
(i)
Kama uko nje ya jengo wakati tetemeko linatokea unashauriwa kubaki nje,
simama mahali pa wazi na uwe mbali na majengo, miti mikubwa, nguzo na
nyaya za umeme na ujikinge kichwani kadri inavyowezekana kwani paa za
nyumba, miti, nguzo na nyaya za umeme vinaweza kudondoka na kuleta
madhara.
(j)
Endapo utakuwa unaendesha chombo cha moto wakati wa tukio la tetemeko
la ardhi unashauriwa usimame kwa uangalifu sehemu salama na usubiri hadi
mitetemo imalizike ndipo uendelee na safari yako kwani tetemeko
linaweza kusababisha barabara au madaraja kukatika.
(k) Endapo utakuwa kwenye maeneo ya miinuko au milima uwe mwangalifu ili kuepuka kuporomokewa na mawe au kuangukiwa na miti,
(l)
Baada ya mitetemo kumalizika endapo itakulazimu kuondoka mahali ulipo
ukiwa katika jengo refu unashauriwa kutumia ngazi badala ya lifti au
kipandishi.
iii Baada ya tukio:
(a)
Wananchi wanashauriwa baada ya tukio kuzima umeme katika majengo ili
kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme kwani mitetemo huenda ikaendelea
tena.
(b)
Kukagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama hayakupata madhara
kama vile nyufa n.k,na kwamba yanaweza kuendelea kutumika na kama
ikibidi basi unashauriwa kuwaita wataalamu wa majengo ili wayafanyie
ukaguzi.
(c)
Endapo utaangukiwa na vitu vizito usijaribu kutumia nguvu nyingi ili
kujinasua kwani hujui vitu hivyo vina uzito kiasi gani, omba msaada kwa
kuita kwa sauti lakini usifanye hivyo mara nyingi ili usipoteze nguvu
nyingi mwilini maana hujui ni lini utaokolewa,
(d) Toa msaada unaowezekana kwa watu walioathirika na tetemeko na utoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika na uokoaji.
0 maoni:
Chapisha Maoni