Serikali imesema vijiji vyote nchini vitakuwa vimepatiwa huduma ya nishati ya umeme katika kipindi cha miaka mitano kupitia Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III).
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokutana na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utafiti wa tetemeko mkoani humo.
Akizungumzia mradi huo wa REA III, Waziri Muhongo aliuelezea kuwa ni mkubwa wa kipekee na kuwa fedha ya kutosha imetengwa ili kuhakikisha mradi huo wa kipekee unakamilika kwa wakati na kama ilivyokusudiwa.
Alisema fedha zilizopo kwa ajili ya mradi huo ni zaidi ya shilingi trilioni moja na kwamba kasi ya usambazaji umeme itaongezeka maradufu kuzidi awamu zilizotangulia.
Aidha, Waziri Muhongo alibainisha kuwa Wakandarasi nane hawataruhusiwa kufanya kazi kwenye Mradi wa REA III kwavile walishindwa kufikia malengo na makubaliano waliyokuwa wamewekeana katika utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II).
“Tunayo majina ya Wakandarasi Nane ambao kazi zao hazikuturidhisha; walishindwa kufikia malengo yaliyokuwa yamewekwa na hivyo hatutoendelea nao,” alisema Profesa Muhongo.
Vilevile Waziri Muhongo aliwaasa wafanyakazi hao wa TANESCO kujiepusha na vitendo vya rushwa ikiwemo kuepuka mazingira yanayoweza kusababisha kuwepo kwa rushwa ili kuwa na ufanisi katika shughuli zao.
Katika kuonesha dhamira hiyo ya kuepuka rushwa, wafanyakazi hao walikula kiapo mbele ya Waziri na kuahidi kwamba hawatajihusisha na vitendo vya rushwa na kuwa watahakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa.
Wakati akiendelea kuzungumza na wafanyakazi hao wa TANESCO, Profesa Muhongo aliwaagiza kuhakikisha wanashughulikia matatizo na malalamiko ya wateja kwa wakati ili kuepusha hali ya kutoelewana na wateja husika.
Profesa Muhongo aliwaagiza kuhakikisha wanatatua matatizo ya wateja. Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi ya wateja kuhusiana na utendaji mbovu wa shirika hilo kote nchini na moja ya malalamiko hayo ikiwa ni ucheleweshwaji wa kuunganishwa na huduma ya umeme jambo ambalo amelikemea vikali.
Mbali na hayo, vilevile Waziri muhongo aliliagiza Shirika hilo kufungua Ofisi katika maeneo ya vijijini hususan pale penye watumiaji wengi wa huduma ya umeme ili kuwaepushia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma kwenye Ofisi za TANESCO ambazo zipo katika makao makuu ya wilaya na mikoa pekee.
“Hatumtendei haki mwananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ambayo angeweza kuipata maeneo anayoishi; ni vyema mkaangalia namna ya kuwa na Ofisi maeneo mbalimbali nje ya makao makuu ya wilaya na mikoa,” alisema.
Alisema ikiwa kuna ugumu wa kuanzisha ofisi katika maeneo ya vijijini, Shirika hilo liangalie namna ya kupeleka huduma katika maeneo hayo kwa ratiba maalum ili wananchi waepuke gharama za kusafiri kufuata Ofisi za Tanesco na badala yake wasubiri siku maalum ambayo watoa huduma watatembelea maeneo husika.
Waziri Muhongo alizungumzia suala la vibarua wanaofanya kazi katika shirika hilo na kuagiza kuwa Bodi ya Wakurugenzi kwa kushirikiana na Menejimenti ya TANESCO kuhakikisha inatatua suala hilo ili kutenda haki kwa wale ambao wamelitumikia shirika hilo kwa miaka mitano hadi 10 bila kuajiriwa.
Aliagiza shirika hilo kuangalia utaratibu wa kuajiri vibarua wenye sifa na wale wasiokuwa na sifa kuwaandalia utaratibu wa kusoma ili waweze kutimiza masharti ya ajira.
Profesa Muhongo alitembelea miundombinu ya Tanesco ambayo imeathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani humo na kujionea hali halisi iliyopo na kuagiza wataalamu waliopo mkoani humo kuhakikisha wanafanya utafiti maeneo wa kina katika maeneo husika na kushauri namna ya kuboresha.
Aidha, alitembelea maeneo yaliyokatiwa huduma ya umeme kwa sababu za kiusalama kutokana na athari ya tetemeko na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo.