Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi Kasiga.
……………………………………………………………………
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali imesema kuwa
inashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kuhakikisha kuwa madereva wanaoendesha magari aina ya malori
ambao wametekwa nyara jana na waasi wa kikundi cha Maimai katika
eneo la Namoyo jimbo la Kivu kusini katika nchi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo wanapatikana wakiwa salama.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa kitengo
cha Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Bi. Mindi Kasiga leo jijini Dar es Salaam alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari juu ya juhudi zinazofanywa na
Serikali katika kuwakoa watanzania waliotekwa nyara.
“Serikali ya Tanzania kwa
kushirikiana na Serikali ya Kongo inaendelea kufanya kila jitihada
kuhakikisha madereva hao wanaachiwa huru haraka iwezekanavyo na
kurudishwa nchini wakiwa salama”
“ Waasi hao wa Maimai wametoa
masaa 24 hadi kufikia leo wawe wamelipwa kiasi cha Dola 4,000 kwa kila
dereva ili waweze kuwaachia huru na kutishia kuwadhuru endapo
hawatapata fedha hizo, hivyo basi Serikali imeendelea kuwa na mazungumzo
na Serikali ya Kongo ili kupata ufumbuzi wa suala hili” alisema Kasiga
Aliongeza kuwa malori yaliyotekwa
nyara ni 12 kati ya hayo nane ni mali ya mfanyabiashara wa kitanzania
Bw. Azim Dewji na mengine ni mali za wafanyabiashara kutoka nchini
Kenya.
Aidha, Serikali imewataka
watanzania kufahamu hali ya usalama wa nchi wanazokwenda ili kujikinga
na matatizo mbalimbali yanayoweza kuwapata wakiwa katika nchi hizo.
0 maoni:
Chapisha Maoni