Na. Sheila Simba,MAELEZO
Jumuiya ya Wanataluma wa Chuo
Kikuu cha Dar Es Salaam (UDASA) imesema kuwa itaendelea kuunga mkono
juhudi za Serikali za kukabiliana na majanga ya asili yanayotokea katika
maeneo mbalimbali nchini, kutoa msaada wa kitaalam na kuwasaidia
waathirika wa majanga hayo.
Aidha, itaendelea kuwahamasisha
wadau mbalimbali waendelee kutoa misaada ya kibinadamu ikiwemo vyakula,
maji safi na salama, makazi ya muda na madawa kwa waathirika wa tetemeko
la ardhi mkoani Kagera ili kuwaepusha na magonjwa ya kuambukiza.
Akizungumza na waandishi wa
habari kwa niaba ya wanajumuiya hao leo jijini Dare Es Salaam na
Mtaalamu wa Jiologia wa chuo hicho Dkt.Elisante Mshihu amesema kuwa
jumuiya yao itaendelea kutoa elimu na taarifa sahihi kwa umma kupitia
tafiti mbalimbali zinazohusu matetemeko ya ardhi kama nyenzo muhimu ya
kukabiliana na majanga hayo.
“Matetemeko ni hali ya kawaida
duniani na kwa hapa kwetu yamekua yakitokea katika mikoa ya
Dodoma,Arusha,Bukoba na Singida ndani ya miaka kumi hivyo ni vyema
wananchi wafahamu namna ya kukabiliana nayo yanapotokea”alisema Dkt
Mshihu
Dkt.Mshihu amesema elimu na
taarifa sahihi ni nyezo madhubuti ya kukabiliana na majanga ya asili
kokote Duniani,na kuongeza kuwa uwekezaji katika elimu ni jambo
linalohitajika kwa sasa hapa nchini.
“Itabidi elimu ya juu na vyombo
vya habari vijengewe uwezo wa kifedha na kitaaluma ili kutimiza
majukumyu yake wakati wa kukabiliana na majanga haya ya asili
”alisisitiza Dkt.Mshihu
Ameongeza kuwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki inapaswa kuelekeza nguu zake katika eneo hilo kwani
kijiografia na kijiolojia inaonyesha Nchi zote wanachama ziko katika
hatari ya kukubwa na majanga ya asili.
Aidha jumuiya hiyo imefungua
akaunti katika bank ya NBC yenye jina la UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
SELF INSURANCE,akaunti namba 040103001175 katika tawi la Chuo Kikuu Cha
Dar Es Salaam,na kuomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia
waathirika wa tetemeko lilitokea mkoani kagera hivi karibuni.
0 maoni:
Chapisha Maoni