Alhamisi, 29 Septemba 2016

Wakandarasi Wanaofunga Nyaya za Umeme Watakiwa na Kuwa na Kibali cha TANESCO

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani akiwaonyesha wananchi wa kijiji cha Mutuka wilayani Babati,  kifaa cha umeme kijulikanacho kama UMETA ambacho kinaweza kuwasha umeme ndani ya nyumba bila kufunga nyaya za umeme. Naibu Waziri alifika katika kijiji hicho kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini ya Awamu ya Pili.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (mwenye suti ya Bluu) akiwahutubia  wananchi wa kijiji cha Magala wilayani Babati,  wakati alipofika katika kijiji hicho ili kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini ya Awamu ya Pili.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati) akivalishwa mgololo na  wananchi wa kijiji cha Magala wilayani Babati,  wakati alipofika katika kijiji hicho ili kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini ya Awamu ya Pili. Wananchi walimvalisha mgololo huo kuonyesha shukrani zao kwa Serikali baada ya kijiji hicho kupata umeme kupitia miradi ya usambazaji umeme vijijini ya Awamu ya Pili.
Na Teresia Mhagama, Manyara

Wakandarasi wote wanaofanya kazi ya wanaofunga nyaya za umeme ndani ya nyumba (wiring),  wametakiwa  kuhakikisha kuwa hawafanyi kazi hiyo mpaka wawe wamepata idhini kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri  wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani  wakati akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika wilaya ya Babati na Mbulu mkoani Manyara.

“Baadhi ya Wakandarasi hawa wanaofanya wiring, wamekuwa wakitoza gharama kubwa ya kutoa huduma hiyo na matokeo yake inapelekea wananchi kuchelewa kuunganishwa na huduma ya umeme,” alisema Dkt Kalemani.

Aliongeza kuwa,  baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakifanya kazi hiyo chini ya viwango na kupelekea matatizo mbalimbali kwa wananchi ikiwemo nyumba kupata hitilafu za umeme na kusababisha majanga kama ya moto na kusisitiza kuwa yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakati huohuo, Dkt. Kalemani aliwaagiza Watendaji wa TANESCO kutoa elimu kwa wananchi  kuhusu faida ya kutumia kifaa kijulikanacho kama UMETA (Umeme Tayari) ambacho huwasha umeme ndani ya  nyumba bila mteja kulazimika kuingia gharama za kufunga nyaya za umeme ndani ya nyumba.

“Kifaa hiki gharama yake ni shilingi 36,000 tu  na kinaweza kutumika kwenye nyumba ya chumba kimoja hadi vitano hivyo TANESCO mnapaswa kutoa elimu kwa wananchi ili wakitumie kifaa hiki,”alisema Dkt.Kalemani.

Kuhusu miradi ya usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili inayokamilika Oktoba 15, 2016, Mhandisi Mushi alisema kuwa miradi hiyo itanufaisha vijiji 96 ambapo wilaya ya Babati  itakuwa na vijiji 56 vitakavyounganishwa na huduma ya umeme, wilaya ya Mbulu itakuwa na vijiji 7, Hanang Vijiji 8 na Simanjiro ni vijiji 15.


Kuhusu vijiji ambavyo havijapata umeme katika Awamu hiyo ya Pili, Dkt Kalemani alisema kuwa vijiji vyote ambavyo havina umeme  nchini vitaunganishiwa umeme kupitia miradi ya REA ya Awamu ya Tatu ambayo utekelezaji wake utaanza mwishoni mwa mwaka huu.

0 maoni:

Chapisha Maoni