Hivi
karibuni kumekuwepo na taarifa iliyotolewa na Taasisi isiyo ya
kiserikali inayofuatilia masuala ya Afya ,Sikika pamoja na baadhi ya
vyombo vya habari kuwa MSD inakabiliwa na upungufu wa dawa na kutoa
takwimu kuwa kuna makopo 173 tu ya dawa aina ya Paracetamol nchini.
Wizara inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa hizi kama ifuatavyo.
Kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016,
MSD ilianza utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja
kutoka kwa wazalishaji kama jitihada za kuhakikisha kuna upatikanaji
endelevu wa mahitaji hayo kwa wananchi.
Wizara kupitia MSD tayari
imepokea makopo 10,000 ya vidonge vya Paracetamol ambayo
yamekwishasambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.Aidha
mkataba kati ya MSD na mtengenezaji wa ndani wenye makopo mengine
138,000 ya vidonge vya Paracetamol yenye ujazo wa vidonge 1,000
umekamilika, ambapo dawa hizo zinategemewa kuanza kupokelewa kuanzia
wiki ya kwanza ya mwezi wa Oktoba 2016.
Aidha, dawa nyingine zilizokuwa
zinahitajika zaidi ambazo ni antibiotics na dawa za kupunguza maumivu
(Ciprofloxacin, Ceftriaxone, , Diclofenac, Co-trimoxazole, Amoxycyline,
Doxycycline na Metronidazole) ziliwasili makao makuu ya MSD na tayari
zimekwisha pelekwa kwenye kanda zote za MSD tayari kwa kusambazwa
kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Kwa sasa hali halisi ya
upatikanaji wa Dawa MSD ni sawa na 53% kwani kati ya dawa muhimu 135
zinazohitajika ghalani kuna aina 71 ya dawa hizo na nyinginezo ziko
kwenye vituo vya kutole huduma. Hali ya upatikanaji wa dawa itaimarika
zaidi mwezi Oktoba mwaka huu hasa kutokana na Bohari ya Dawa kutumia
mikataba ya muda mrefu na washitiri (Framework contracts) ili kuimarisha
upatikanaji wa dawa wa haraka, pindi zinapohitajika kulingana na fedha
zinazopatikana.
Vilevile tunapenda kutoa taarifa
kwa umma kuwa dawa za Miradi Msonge, ambazo zinatibu na kuzuia magonjwa
ya Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu, Ukoma, kichaa cha mbwa, uzazi wa mpango
na chanjo mbalimbali zipo za kutosha kwenye Bohari zetu.
Kadhalika, Wizara inapenda kutoa
taarifa kuwa hali ya upatikanaji wa chanjo nchini utaimarika zaidi
kuanzia tarehe 2 Oktoba, 2016 baada ya kupokea shehena mpya. Hata hivyo,
Wizara inawaomba Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuangalia mwenendo wa
shehana zao na kutoa mgawo mpya kwenye maeneo yenye upungufu (stock
redistribution)pale kadhia hii inapotokea.
Dkt. Mpoki Ulisubisya
KATIBU MKUU-AFYA
27 Septemba, 2016
0 maoni:
Chapisha Maoni