Alhamisi, 15 Septemba 2016

(JWTZ) KIKOSI CHA NCHI KAVU MSANGANI LACHANGIA MADAWATI 200 MKOA WA PWANI

jwt1
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimshukuru Kamanda wa jeshi  la  nchi kavu kikosi cha Msangani ,Brigadia Jeneral Jairos Mwaseba baada ya jeshi  hilo kuchangia madawati 200 katika mkoa wa Pwani. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
jwt2
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, wa katikati ,ambapo kulia  ni kamanda wa jeshi la nchi kavu kikosi cha Msangani Brigedia Jenerari  Jairos Mwaseba na kushoto ni Brigedia Jenerari  A .S.Bahati wakiwa wameketi kwenye moja ya madawati ambayo jeshi  hilo limechangia Mkoani Pwani. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
jwt3
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akipokea moja ya madawati kutoka kwa  Kamanda wa jeshi  la  nchi kavu kikosi cha Msangani ,Brigadia Jeneral Jairos Mwaseba baada ya jeshi  hilo kuchangia madawati 200 katika mkoa wa Pwani, Kulia ni Brigedia Jenerari  A .S.Bahati (Picha na Mwamvua Mwinyi)
…………………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU  wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amepokea madawati 200 kutoka kwa jeshi la nchi kavu kikosi cha Msangani,ambayo yatasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa madawati mkoani hapo .
Aidha sekretarieti ya mkoa imefanya jitihada za makusudi kuomba wadau mbalimbali kuchangia upatikanaji wa madawati ambapo imepata madawati 1,000.
Akikabidhiwa madawati hayo na brigadia general JM.Mwaseba pamoja na brigadia general AS.Bahati kwa niaba ya mkuu wa jeshi la nchi kavu Msangani,meja general James Mwakiborwa,mhandisi Ndikilo ,alilishukuru jeshi hilo kwa kuunga mkono sekta ya elimu.
Alieleza kuwa kabla ya agizo la Rais John Magufuli la kuondoa changamoto ya uhaba wa madawati katika shule za msingi na sekondari,katika mkoa huo kulikuwa na upungufu wa madawati 5,451 katika shule za sekondari.
Alisema upande wa shule za msingi upungufu wa madawati ulikuwa ni 43,507 lakini kwasasa wanashukuru tatizo hilo linaelekea kumalizika na kuwa historia.
Mhandisi Ndikilo alisema wilaya ya Mkuranga ,Rufiji na Mji wa Kibaha ndio zilizokuwa na mapungufu makubwa ya madawati lakini wakurugenzi wa halmshauri za wilaya hizo walijipanga kukabiliana na hali hiyo.
Hata hivyo alisema mchango huo utawezesha wanafunzi kuondokana na kero ya awali waliyokuwa wakiipata hali iliyokuwa ikisababisha kushindwa kusoma katika mazingira bora.
“Kwa niaba ya mkoa nawashukuru jeshi la nchi kavu ,mmeonyesha ni sehemu ya jamii ya mkoa,mfikishieni salamu zangu za dhani kwa meja general Mwakiborwa,tutaendelea kuwaenzi na tunawaombea muendelee kulinda amani ya nchi”alisema.
Alitaja mikakati iliyowekwa kufanikisha suala hilo,kuwa ni pamoja na wakurugenzi kuunda kamati mbalimbali za kufuatilia utengenezaji wa madawati,mbao na magogo yaliyokamatwa na askari wa maliasili vilielekezwa kutengeneza madawati.
Mhandisi Ndikilo alisema halmashauri zilitumia vyanzo vyao vya mapato,kutafuta wadau wa ndani na nje ya wilaya na mkoa,kuitisha harambee,kuhamasisha jamii na kukarabati madawati yaliyochakaa kidogo.
Awali katibu tawala wa mkoa huo,Zuberi Samataba alieleza miongoni mwa wadau waliojitokeza kuchangia zoezi hilo mkoani humo ni jeshi la nchi kavu na ubalozi wa China.
Wengine ni kampuni ya goodwill Tanzania ltd ya Mkuranga,mamlaka ya bandari Tanzania ,taasisi mbalimbali binafsi na za umma,kampuni ya tigo.
Samataba alisema madawati zaidi ya 1,000 kutoka kwa wadau hao yatagawiwa katika shule mbalimbali kulingana na mahitaji.
Alisema sekretriet ya mkoa inaendelea kuwasiliana na wadau wengine kuendelea kuunga mkono juhudi za kufanikisha upatikanaji wa madawati.
Brigadia general JM.Mwaseba ,alisema wakati mkoa ukiendelea na juhudi zake kufanikisha adhma hiyo jeshi hilo limejitolea kutoa madawati hayo ili kumuunga mkono rais Magufuli .
Alisema madawati hayo yametengenezwa katika kiwanda cha nyumbu chini ya brigadia jeneral AS.Bahati.
Afisa elimu mkoani Pwani,Yusuph Kipengele alisema mkoa umeshakamilisha madawati ya shule za msingi na sekondari kwa asilimia 99.
Alisema mojawapo kati ya matokeo ya elimu bila malipo ni ongezeko la wanafunzi na hivyo kusababisha ongezeko la mahitaji ya miundombinu na samani ikiwemo madawati .
Kipengele alieleza kuwa upande wa sekondari awali mkoa ulikuwa na mahitaji ya madawati 47,276 yaliyokuwepo 42,795 upungufu ulikuwa 4,481 sawa na asilimia 10.47.
Kipengele alisema shule za msingi mkoa ulikuwa na mahitaji ya madawati 92,586 yaliyokuwepo ni 61,318 upungufu ulikuwa ni madawati 31,268 sawa na asilimia 33.77.

0 maoni:

Chapisha Maoni