Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ambao mara nyingi walikuwa wakifuata matibabu yasiyopatikana hapa nchini ama kutokana na kutokuwepo wataalamu au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika.
Katika kutekeleza hilo, Septemba 25, 2016, Hospitali ya Taifa Muhimbili itapeleka watalaamu saba nchini India katika Hospitali ya Apollo iliyopo New Delhi ili wakajifunze kwa njia ya vitendo jinsi ya kufanya upasuaji na upandikizaji wa kifaa cha usikivu kwa watu wazima na watoto. Wataalamu hao ni pamoja na madaktari bingwa wawili wa upasuaji wa pua, koo na masikio, wauguzi wawili wa chumba cha upasuaji, mtalaam mmoja wa kupima usikivu pamoja na watalaam wawili wa kufundisha jinsi ya kuongea hususani kwa watoto waliozaliwa na tatizo hilo.
Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kifaa cha usikivu ni watoto wadogo. Hivyo tunatarajia huduma hii kusaidia watoto wengi hapa nchini na pia kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani ya nchi.  
Gharama za kupandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja ni kati ya shilingi milioni 80 hadi 100 anapopelekwa nje ya nchi wakati mgonjwa mmoja anayepandikizwa figo nje ya nchi pia hugharimu kiasi cha shilingi milioni 40 hadi 60. Uwepo wa huduma hizi hapa nchini utawezesha watanzania wengi kupata huduma hii na kwa gharama nafuu zaidi na kupunguza mzigo kwa Serikali wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwani gharama za matibabu zitapungua kwa zaidi ya asilimia 50.
Wataalam hawa wanatarajia kurejea hapa nchini Oktoba 28, 2016 tayari kuanza kutoa huduma hiyo. Mapema mwezi huu Hospitali ya Taifa Muhimbili ilipeleka nchini India wataalamu 18 wa fani mbalimbali kwa ajili ya kujengewa uwezo wa upandikizaji figo kwa watu wenye matatizo ya figo ambapo timu hiyo inatarajia kurejea mwishoni mwaka huu.
Gharama za kupeleka timu zote mbili ya upandikizaji wa figo pamoja na upandikizaji wa kifaa cha usikivu ni shilingi milioni 528 zikijumuisha gharama za mafunzo, nauli, fedha za kujikimu pamoja na gharama nyingine za mafunzo. Fedha hizi zote zitalipwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kujenga uwezo wa watalaamu wake.
Aidha Hospitali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 3.4 ili kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 12 hadi 20, na sasa hivi tunavifanyia ukarabati viliyokuwepo 12 na kuweka vifaa vipya katika vyumba vya upasuaji vitakavyoongezwa. Eneo la huduma za uchujaji wa damu kwa wagonjwa wa figo litapanuliwa na kuongeza vitanda kutoka 17 vya sasa hadi vitanda 42 sambamba na kuongeza mashine zake kufikia 42 na kuweka mtambo wa kuchuja maji (water-treatment plant).
 Hospitali itaongeza pia vyumba vya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu vipya vinne (ICUs) vikiwa na jumla ya vitanda 40 na kuviwekea vifaa vipya pamoja na vyumba vinne vya kupokea wagonjwa baada ya kutoka ICU (step-down ICU) na kabla ya kwenda kwenye wodi za kawaida navyo vitakuwa na vitanda 40. Aidha Ukarabati na ujenzi wa miundo mbinu hii unaendelea na unatarajiwa kuwa umekamilika ifikapo mwishoni mwa Disemba 2016.
(Pichani) Kaimu-Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru 
ApolloEneo la jengo la Hospitali ya Apollo ya India