Posted by Esta Malibiche on Sept30.2016
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, inatoa taarifa kuwa, tarehe 1 Oktoba ya
kila mwaka, ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani. Katika
siku hii, Tanzania inaungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa
Mataifa kuadhimisha Siku hii kwa mujibu wa Azimio la Umoja wa Mataifa
Na. 49 la mwaka 1991.
Maadhimisho ya siku ya wazee
duniani ni moja kati ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN)
katika kutambua na kuhamasisha jamii kuweza kulinda na kutetea haki za
wazee duniani kote. Umoja wa Mataifa umetenga siku hii kwa lengo la
kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili wazee;
na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya
waishi maisha ya heshima, hadhi, na kuthaminiwa utu wao.
Kila mwaka, Maadhimisho haya huwa yanabeba Kauli Mbiu yenye ujumbe mahsusi. Kwa mwaka 2016 Kaulimbiu inasema “Zuia Unyanyasaji dhidi ya Wazee”.
Kaulimbiu hii inahimiza Serikali, jamii, na wadau wengine kutafakari na
kuweka mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili, mauaji, ubaguzi
na dhuluma dhidi ya wazee; vitendo ambayo ni kinyume dhidi ya haki za
binadamu.
Maadhimisho haya kwa mwaka 2016
yanafanyika Kitaifa katika wilaya ya Mbalali, mkoani Mbeya. Kilele cha
maadhimisho haya kitajumuisha shughuli mbalimbali ikiwemo huduma ya
upimaji wa hiari wa afya na ushauri kwa wazee, michezo na maonesho ya
bidhaa na kazi mbalimbali zinazofanywa na wazee.
Katika kipindi hiki cha
Maadhimisho hatuna budi kuenzi na kudumisha mila na desturi nzuri za
kuwaenzi wazee kwa kutambua kuwa wazee ndiyo chanzo cha urithi wa
historia ya nchi, washauri wa familia na jamii, watu wenye hekima, na
walezi katika jamii. Hivyo jamii inaowajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee
katika kupata huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua pale
ambapo mzee ananyanyashwa au kutendewa isivyostahili.
Erasto T. Ching’oro
Msemaji wa Wizara
30/9/2016
0 maoni:
Chapisha Maoni