Posted by Esta Malibiche on Sept29.2016 in NEWS
SERIKALI ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli imetenga kiasi cha sh. Bil. 100
katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa
viwanja mbalimbali vya ndege nchini.
Rais Dk. Magufuli alisema hayo
juzi katika sherehe za uzinduzi wa ndege mbili za Shirika la ndege la
Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na
serikali, kwenye Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), ambapo viwanja hivyo vitaboreshwa ili kuwezesha ndege hizo kutua
bila wasiwasi.
Mhe. Rais akifafanua zaidi,
alisema , kiwanja cha ndege cha Nduli kilichopo umbali wa kilometa 13
Kaskazini Mashariki mwa Manispaa ya Iringa, ambacho kipo kwenye kiwango
cha lami kitakarabatiwa, ili ndege hizo zitue na kupaa bila tatizo.
Dk. Magufuli alisema, kiwanja cha
Nduli Iringa ni kiunganishi kikubwa na JNIA na kitatumika kupeleka
watalii wanaokwenda kutembelea mbuga ya wanyama ya Ruaha, wakitokea
Mataifa mbalimbali duniani.
Alisema mbali na kiwanja hicho
cha Nduli, pia kiwanja cha Musoma kitawekwa lami, ili nacho kiwe moja ya
maeneo ndege hiyo itakwenda, na kurahisisha usafiri wa watalii
watakaokwenda kwenye mbuga ya wanyama ya Serengeti. Kwa sasa kiwanja cha
Musoma kipo katika kiwango cha changarawe na kinatumika kwa ndege
mbalimbali kutua na kupaa.
Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanja
cha ndege cha Nduli, Bi. Hannah Kibopile, kiwanja hicho kinapokea ndege
ndogo zaidi ya saba zenye uwezo wa kubeba abiria 13, na kati ya hizo
tatu zipo kwenye ratiba maalum ya kila siku na zilizosalia ni za
kukodishwa na nyingine zinakwenda mbuga ya wanyama ya Ruaha.
Bi. Kibopile alisema ndege zinazotua kwenye kiwanja hicho zinatoka Jijini Dar es Salaam, Sumbawanga, Songea na Mbuga ya Ruaha.
Naye Kaimu Meneja wa Musoma, Bi.
Faraja Mayugwa amesema kiwanja hicho kinapokea ndege zaidi ya nne kwa
siku na nyingi zinakuwa za kukodi zinazopeleka watalii mbugani.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli
alisema “Hii ndege inaweza kutua katika kiwanja cha aina yeyote; na
serikali itaendelea na ukarabati wa viwanja vya ndege vya pembezoni, ili
viwe katika kiwango, ambacho ndege hizi zitatua na kuruka bila
wasiwasi,”.
Akifafanua zaidi Dk. Magufuli
alisema serikali inatarajia kununua ndege nyingine kubwa mbili zenye
uwezo wa kubeba abiria 160 na 242, ambazo zitaanzia safari zake kwenye
JNIA kwenda sehemu mbalimbali duniani kama China au Marekani moja kwa
moja, ikiwa ni lengo la kupata abiria hao, ambao wengi wao watakuwa
watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali. Bombardier
inauwezo wa kubeba abiria 76.
Naye Waziri wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof Makame Mbarawa awali wakati
akimkaribisha Mhe. Rais kuzungumza na wananchi katika ghafla hiyo ya
uzinduzi wa ndege, alisema kwa kuanzia ndege hizo zitatua kwenye viwanja
11 vya ndege, ambavyo ni Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), Kilimanjaro (KIA), Zanzibar (AAKIA), Mwanza, Dodoma, Arusha,
Bukoba, Kigoma, Tabora, Mbeya na Mtwara. Pia ndege hiyo itakwenda
Comoro.
Mhe. Prof. Mbarawa ameiagiza
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuendelea kufanya upembuzi
yakinifu kwa kuangalia viwanja vingine vya ndege, ambavyo ndege hizi
zitakwenda.
0 maoni:
Chapisha Maoni