Alhamisi, 29 Septemba 2016

WAFUGAJI WATAKIWA KUACHANA NA UFUGAJI WA UFAHARI

Posted by Esta Malibiche on Sept29.2016 in NEWS

index
Na Mwamvua Mwinyi
WAZIRI mkuu ,Kassim Majaliwa ,amewataka wafugaji hususan wamang’ati,wamasai na barbeig nchini kufuga kisasa na kuachana na ufugaji wa kuzurura na mifugo bila manufaa .
Aidha amesema wafugaji hao wanapaswa kupatiwa elimu juu ya  umuhimu wa kuuza mifugo yao kwa tija  badala ya kuona  ufahari wa kukaa na kundi kubwa la mifugo.
Akizungumza na wananchi wilayani Kibiti,alieleza kuwa wafugaji wanatakiwa kuelimika kuhusiana na suala hilo ili kupunguza ama kuondoa tatizo la migogoro ya  wakulima na wafugaji katika maeneo mengi hapa nchini.
Majaliwa amewaasa wafugaji  waridhie kuuza mifugo yao minadani  wasikae nayo na kuhamahama nayo   kiholela bila mpangilio kwenye vijiji na wilaya zisizo na maeneo kwa ajili ya mifugo.
Ameongeza kuwa  kuna kila sababu ya kuwashauri wauze baadhi ya Ng’ombe wao  na kubaki na Ng’ombe wachache kuliko kukaa na kundi kubwa.
“Wafugaji ridhieni kuwauza Ng’ombe,Mbuzi,Kondoo zenu ,msikae nao kuzurula nao misituni,uzeni mbakie na mifugo mtakayoimudu pasipo kusababisha changamoto kwenye jamii”
“Ndio maana serikali inasisitiza viwanda ,na tunakaribisha wajenzi wa ndani na nje ya nchi ,waje wajenge viwanda vingi ikiwemo vya kusaga nyama za ng’ombe ,kondoo ili ng’ombe hawa waishie viwandani”
Hata hivyo ameeleza kuwa serikali imewakataza  wafugaji wote kuwa ni marufuku kupeleka mifugo  kwenye  mazao ya wakulima ili kuondokanana tatizo kubwa la migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Majaliwa ametoa rai kwa  wafugaji waridhie mpango wa serikali wa matumizi bora ya ardhi .
Amesema haiwezekani ng’ombe atembee hapa hadi Morogoro hata akichinjwa itakuwa sio nyama nzuri hivyo amewaomba waondokane na kasumba ya kutembeza ng’ombe umbali mrefu kwani ni ufugaji usio na tija.
Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia mpango wa matumizo bora ya ardhi kwa kuhakikisha wanatafuta maeneo ya wafugaji ambayo yana maji ili kujenga malambo na majosho.
Amewataka viongozi hao  kusimamia suala la wakulima na wafugaji kwenye maeneo yao badala ya kusubiri liibuliwe kwenye majukwaa licha ya kuwa tayari serikali imewapa maagizo ya kusimamia suala hilo.
Waziri mkuu amesema wapo baadhi ya wenyeviti wa vijiji na watendaji wakidaiwa kuchukua rushwa na kuingia idadi ya mifugo ambayo hairuhusiwi hivyo ni lazima wawachukulie hatua.
Ameongeza kuwa tatizo la migogoro hiyo ni sugu na kubwa kwani linachangiwa na viongozi na watendaji wenyewe kujihusisha kuingiza mifugo hiyo na kupelekea kukua kwa changamoto hiyo.
Mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa hapa nchi ambayo moja ya changamoto sugu ni migogoro ya wakulima na wafugaji hasa wilaya ya Bagamoyo,Kibiti,Rufiji,Kisarawe na Kibaha.

0 maoni:

Chapisha Maoni