Alhamisi, 29 Septemba 2016

TAASISI YA UTAFITI WA MAGONJWA YA BINADAMU – NIMR YAANDAA KONGAMANO LA WATAFITI


Posted by Esta Malibiche on Sept29.2016 in NEWS
1
Dk. Mwele Malecela Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es salaam wakati alipotangaza kongamano kubwa la watafiti litakalofanyika tarehe 4 mpaka 6 Oktoba 2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
2
Dk. Mwele Malecela Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati alipokuwa akizungumza nao leo, Kulia ni Dk. Julius Massaga Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti/Mtafiti Mkuu wa NIMR.
………………………………………………………………………
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ilianzishwa kwa Sheria namba 23 ya mwaka 1979.  Katika kipindi cha miaka 29 iliyopita Taasisi imekuwa ikiandaa Kongamano la sayansi kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha watafiti, watoa huduma za afya,  watunga sera, wakufunzi, wahisani na wadau wengine wa afya kuwasilisha na kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali za afya.
NIMR imeandaa Kongamano lake la 30 kuanzia tarehe 4 mpaka 6 Oktoba 2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Kongamano hilo atakuwa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Ufunguzi utakuwa saa 3 asubuhi ya Oktoba 4, 2016.
Mada kuu ya Kongamano hilo ni “Uwekezaji katika tafiti zenye ubunifu ili kufikia malengo endelevu ya dunia.” Jumla ya mada 220 zitawasilishwa na kujadiliwa katika Kongamano hili la Siku 3. Mada hizo zitakuwa katika maeneo yafuatayo:
  1. Mkakati wa kuboresha afya ya uzazi, ya mama, watoto wachanga na vijana.
  2. Magonjwa sugu yasiyoambukiza na changamoto zake
  3. Kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya UKIMWI, kifua kikuu na malaria
  4. Usalama wa Maji, Usafi wa mazingira na usafi binafsi.
  5. Mkakati wa afya moja katika kudhibiti magonjwa ya milipuko
  6. Magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele
Mada hizi zinalenga katika kujadili haja ya kuwekeza katika tafiti za mifumo ya utoaji huduma, magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza na tabia na shughuli za kibinadamu zinazochangia kuwepo kwa maradhi. Mikakati ya kufikia Malengo Endelevu ya Dunia itajadiliwa na mapendekezo kuwasilishwa kwa Serikali na wadau wengine.
Ndugu waandishi, NIMR inaamini kwamba watafiti wana michango mkubwa katika kuleta maendeleo kupitia matokeo ya tafiti mbalimbali wanazofanya juu ya magonjwa ya binadamu. Ni kwa msingi huo basi, Taasisi inasisitiza kwamba kila mtafiti ana jukumu la kuwasaidia Watanzania kufikia malengo endelevu ya dunia kwa kuepuka magonjwa.
Pamoja na uwasilishwaji na majadiliano katika mada mbalimbali, Taasisi imeandaa:
  1. Maonesho ya bidhaa zitokanazo na tafiti, taarifa za kitafiti, machapisho, vifaa vya utafiti, vyenzo za kutoa huduma za afya
  2. Mikutano maalum miwili itakayojadili
    1. Wanawake katika Sayansi
    2. Mikakati ya kuhamasisha ufadhili wa Tafifi kwa Wadau wa ndani ya nchi
  3. Tuzo kwa wanasayansi katika zikiwemo: (i) Mtafiti Bora wa Afya Afrika; Mtafiti Bora wa Afya Tanzania; Mtafiti Mbunifu wa Mwaka na Mtafiti Bora katika kuchapisha Maandiko ya Kitafiti. Taasisi pia itamzawadia Kiongozi Mashuhuri wa Tanzania aliyetoa mchango mkubwa katika kuinua na kuimarisha tafiti za afya nchini.
Jumla ya Washiriki 300 wamejisajili kuhudhuria kongamano hili. Washiriki wanatoka katika nchi zifuatazo: Afrika Kusini, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Australia, Denmark, Ubeljiji, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Uswis, Kanada, Sweden, Norway, Marekani, Bangladesh, Thailand na Tanzania
Taasisi za Tanzania ni pamoja na: Taasisi ya Afya Ifakara, Vyuo Vikuu vya Tiba na Sayansi za Afya vya Muhimbili na Bugando, Chuo Kikuu cha KCMC, Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kilimanjaro, Chuo Kikuu Dodoma, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia, Hospitali ya Rufaa KCMC, AMREF Health Africa, Hospitali ya Rufaa Amana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.
NIMR ni taasisi utafiti wa magonjwa ya binadamu; yenye majukumu makuu yafuatayo:
  • i). Kuratibu, kukuza na kuendeleza utafiti wa afya nchini.
  • ii). Kufanya utafiti wa afya ili kupunguza magonjwa yanayosumbua jamii.
  • iii). Kufaya utafiti wa tiba asilia na tiba mbadala.
  • iv). Kusajili tafiti za afya zinazofanywa nchini.
  • v). Kuwajengea uwezo watafiti wa Kitanzania katika kufaya tafiti za afya.
  • vi). Kukuza matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya.
Taasisi ina vituo 15 ambapo 8 ni vituo vikubwa na vituo vidogo 5.
Nawaalika watanzania wote kuhudhuria Kongamano hili ili kupata taarifa za uhakika kuhusu tafiti za afya zinazofanywa na Taasisi zetu. Bila kusahau, napenda kuishukuru Wanahabari wote mliofika hapa kwa kutenga muda wenu kutupa fursa hii adimu kuweza kuwasiliana na Watanzania wenzetu kuhusu shughuli zetu na hususan kuhusu Kongamano hili. Natambua vyombo vya habari ni njia nzuri ya kufikisha ujumbe kwa haraka, na pia nyenzo muhimu katika kuhamasisha matumizi ya matokeo ya tafiti za afya. Tunawakaribis sana katika Kongamano letu!
Kwa mawasiliano zaidi:
Mkurugenzi Mkuu
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
Barabara ya Barack Obama
S.L. B. 9653, Dar es Salaam
Simu: +255222121400; Nukushi: +255222121360
Baruapepe: info@nimr.or.tz

0 maoni:

Chapisha Maoni