Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi
Nyanza Road Construction inayojenga barabara ya Furahisha hadi Pasiansi
KM 2.8 wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo, jijini Mwanza.
Mkandarasi wa kampuni ya Nyanza
Road Construction inayojenga barabara ya Furahisha hadi Pasiansi akitoa
maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo jijini Mwanza.
…………………………………………………………………
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya
Beijing Construction Engineering Group anayejenga uwanja wa ndege wa
Mwanza kumaliza kazi ya upanuzi wa uwanja huo ifikapo mwezi Februari
Mwakani.
Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo
alipokuwa akikagua kazi ya ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa
Mwanza pamoja na daraja la watembea kwa miguu lililopo maeneo ya
furahisha, jijini Mwanza.
Profesa Mbarawa amesema kuwa
kukamilika kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja huo kutaimarisha hali ya
usafiri wa anga kwa wakazi wa Mwanza na mikoa mingine na hivyo kukuza
shughuli za kibiashara nchini.
“Hakikisheni upanuzi wa uwanja wa
ndege huu unakamilika haraka ili kurahisisha na kuboresha huduma za
usafirishaji kiwanjani hapa”, amesema Waziri Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa amemtaka
mkandarasi wa kampuni ya Nyanza Road Construction kumaliza kwa wakati
upanuzi wa barabara ya ‘Mwanza-Airport’ eneo linaloanzia Ghana Quarters
hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza KM 9.15 pamoja na daraja la watembea kwa
miguu la furahisha ili kukuza uchumi na kupunguza kero ya msongamano wa
magari katika jiji la Mwanza.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amewataka wananchi wa Mwanza kutoharibu miundombinu ya barabara
na madaraja ambayo Serikali inatumia gharama kubwa katika utengenezaji
wake.
“Naomba muitunze na kuithamini
miundombinu hii kwani Serikali inatumia gharama kubwa katika kutengeneza
na kukarabati”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Ujenzi wa uwanja wa ndege wa
Mwanza ni mkakati wa Serikali kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo
unaboreshwa kuwa wa kisasa na wa kimataifa ili kuwezesha ndege kubwa
kutua kwa wingi na kuwa kiungo muhimu kwa mikoa 10 ya kanda ya Ziwa na
Kati.
0 maoni:
Chapisha Maoni