Afisa Msimamizi wa Miradi ya Kuweka na Kukopa kutoka Shirika
la Uhamasishaji Hifadhi Kisarawe (UHIKI) , Vuai Shame akiongea na
waandishi wahabari (hawapopichani) juu ya umuhimu wa vijana waliohitimu
mafunzo ya ufundi chini ya mradi wa Uwezeshaji Vijan aKiuchumi (YEE)
kupata elimu ya utunzaji wa fedha pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa
ajili waweze kuimarisha biashara zao.
Vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi chini ya mradi wa
Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) wakiwa na vyeti vya utambulisho wa
kikundi chao kilichosajiliwa kwajina la YEE Tailoring and Decoration
Group na Halmashauri ya Manispaa ya Kisarawe,nyuma kulia ni Mratibu wa
Mradiwa YEE Kanda yaMashariki, Adolf Jeremiah.
……………………………………………………………….
……………………………………………………………….
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Kisarawe.
Shirika la Uhamasishaji Hifadhi
Kisarawe (UHIKI) limetoa mafunzo ya kuweka na kukopa fedha kwa vijana
waliohitimu mafunzo ya ufundi chini ya mradi wa Uwezeshaji Vijana
Kiuchumi (YEE) ili kuwaelimisha jinsi ya kutunza fedha zao.
Mafunzo hayo yametolewa leo
katika Kijiji cha Kauzeni, Kata ya Kibuta wilayani Kisarawe ambapo
vijana wamefundishwa jinsi ya kupanga, kuchagua na kusimamia shughuli
yoyote inayofanywa kwa ajili ya kujiingiza kipato pamoja na umuhimu wa
kujiwekea akiba.
Afisa Msimamizi wa Miradi ya
Kuweka na Kukopa – Kisarawe, Vuai Shame amesema kuwa kuna umuhimu wa
vijana kupata elimu juu ya utunzaji wa fedha pamoja na upatikanaji wa
mikopo ili waweze kuimarisha biashara zao na kuona faida inayopatikana
kutokana na biashara hizo.
“Kazi ya UHIKI ni kuwasimamia
vijana ili waweze kuunda vikundi vya kuweka na kukopa fedha
zitakazowasaidia kuendeleza biashara zao, mpaka sasa tumefanikiwa kuwa
na vikundi 27 vya vijana vilivyopo katika kata 4 za wilaya yetu lakini
bado tunaendelea kuwahamasisha vijana wengine kufanya hivyo kwani
vikundi vina faida”, alisema Shame.
Afisa huyo ameongeza kuwa kwa
sasa wameamua kuwasajili vijana katika makundi kulingana na fani
walizosomea ili kuwarahisishia kupata mikopo au misaada kutoka sehemu
mbalimbali pamoja na kupanua uwanja wa fursa za kupata tenda kwa wingi.
Aidha, Shame ameishukuru
Serikali kwa kuwa bega kwa bega na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
katika kuhakikisha wanawasaidia vijana kujikwamua kutoka kwenye lindi la
umasikini kwa kuwapa mikopo vijana walio katika vikundi hivyo ili
waimarishe biashara zao na kujiongezea vipato.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha
hisa cha Jitegemee, Yassin Omary amesema kuwa walianzisha kikundi hicho
mnamo Februari 2 mwaka huu baada ya kuhitimu elimu ya ufundi chini ya
mradi wa YEE ambapo hadi sasa wamefanikiwa kuwekeza jumla ya hisa
1,621,000 zinazowawezesha kujikopesha wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya
kutatua changamoto zao.
“Kujiunga kwenye vikundi vya
namna hii kuna umuhimu hasa kwa sisi vijana ambao biashara zetu bado
changa kwani vinatupa uwezo wa kukopa fedha pale biashara inapoyumba au
pale unapotaka kuongeza mtaji kwa ajili ya kuinua biashara yako”,alisema
Omary.
UHIKI ni shirika lisilokuwa la
kiserikali lililoanzishwa mwaka 2009, ni moja kati ya mashirika
yanayowasaidia vijana waliopo chini ya mradi wa YEE unaofadhiliwa na
Umoja wa Ulaya (EU) na kuratibiwa na shirika la Plan International
katika kuunda vikundi vya kuweka na kukopa fedha.
0 maoni:
Chapisha Maoni