Posted by Esta Malibiche on Sept29.2016 in NEWS
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja
Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akiongea na wawakilishi wa familia
waliopoteza ndugu zao (hawapo pichani) kwa tetemeko la ardhi lililotokea
mapema Septemba 10 mwaka huu Bukoba mjini wakati wa kukabidhiwa
rambirambi iliyotolewa na Serikali milioni 17 pamoja na kampuni ya simu
ya Halotel ambayo imetoa shilingi milioni 15.kulia ni Mkurugenzi wa
Idara ya Maafa
Yusta Jonas mkazi wa Hamugembe
Manispaa ya Bukoba akipokea rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambayo imetolewa na Serikali pamoja
na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
Mzee Vedasto Kato kutoka mtaa wa
Hamgembe Manispaa ya Bukoba akipokea rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa
wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambayo imetolewa na Serikali
pamoja na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja
Jenerali Mstaafu Salum Kijuu (katikati aliyekaa) akiwa katika picha ya
pamoja na wawakilishi wa wanafamilia waliofiwa na ndugu zao wakati wa
tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu.
(Picha na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba)
…………………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba
Familia 15 zilizofiwa na ndugu
zao 17 wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani wa Kagera
zimepokea rambirambi ya jumla ya shilingi milioni 32 ikiwa ni mkono wa
faraja kwa msiba uliwafika familia hizo na taifa kwa ujumla.
Rambirambi hiyo imetolewa mjini
Bukoba na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kwa
niaba ya Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya simu za mkononi nchini
ya Halotel ili kuwashika mkono wafiwa hao kwa kupoteza ndugu na jamaa
zao.
Katika rambirambi hiyo, Serikali
imetoa shilingi milioni 17 na kampuni ya simu ya Halotel imetoa shilingi
milioni 15 ambapo kila familia ya mfiwa amepokea shilingi 1,000,000
kutoka Serikalini na shilingi 885,000 kutoka kampuni ya Halotel.
Hatua hiyo inapelekea kila
familia ya mfiwa kupokea jumla shilingi 1,885,000 ambapo familia mbili
zilizopoteza ndugu zao wawili wawili wamepokea jumla ya shilingi
3,770,000 ikiwa ni rambirambi kwa kila ndugu aliyefariki wakati wa tukio
hilo la tetemeko la ardhi.
Akikabidhi rambirambi hiyo kwa
familia hizo, Mkuu wa Mkoa wa huo akiwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya
Maafa mkoa Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema kuwa Serikali imetoa
rambirambi hiyo kwa lengo kuwapa pole wafiwa hao kutokana na kuwapoteza
ndugu na jamaa zao wakati wa tetemeko hilo lililotokea Septemba 10,
mwaka huu.
Katika kuwahakikishia usalama na
utunzaji wa fedha walizopokea wafiwa hao, Mkuu wa mkoa huo amewaasa
wasikuwa na akaunti wafungue akaunti katika benki yeyote ili waweze
kuziweka fedha hizo walizopokea ili kuwahakikishia usalama badala ya
kutembea nazo mkononi.
Wawakilishi wa familia
zilizopokea rambirambi hiyo ni pamoja na Vedasto Katto (Hamugembe),
Geofrey Gerald (Mafumbo), Alex Felix (Hamugembe), Orestus Aron
(Hamugembe), Justa Mkalisa Jonas (Hamugembe), Albert Tibangayuka
(Barabara ya Sokoine), Sheikh Mikidadi Abdallah (Hamugembe) na Maria
Stella John (Hamugembe).
Wanafamilia wengine waliopokea
rambirambi ni Swidick Miyonga (Hamugembe), Jackson Evason (Rwamishenye),
Jasson Rugemalila (Rwome), Augustine Muhigi (Rwome), Edson S. Rwetabula
(Kashenye), Anitha Evalista (Omurushaka) na John Mulokozi Kahangwa
(Kanyigo-Kikukwe).
Aidha, mkuu huyo wa mkoa
ameishukuru Kampuni ya simu ya mkononi ya Halotel kwa kuunga mkono
juhudi za Serikali katika kutoa rambirambi na kuwafuta machozi familia
za marehemu hao na kuwahakikishia kuwa Serikali inathamini mchango wao
kwa jamii.
Akitoa neno la shukrani mara
baada ya kupokea rambirambi hiyo kwa niaba ya wafiwa wenzake, Mzee
Vedasto Kato kutoka mtaa wa Hamgembe Manispaa ya Bukoba ametoa shukrani
kwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona
haja ya kuwashika mkono baada ya kupoteza ndugu zao.
“Tunaishukuru Serikali kwa
kutujali wafiwa tuliopoteza ndugu zetu wakati wa tetemeko la ardhi
lililotokea katika mkoa wetu mwezi huu na kutuonea huruma katika kipindi
hiki kigumu kilichotuachia majonzi makubwa katika familia zetu” alisema
mzee Vedasto.
Mzee Vedasto amesema kuwa hatua
iliyochukuliwa na Serikali katika kuwapa mkono wa pole imewapa faraja na
ameiomba Serikali kuendelea kuwajali wananchi wake kama ilivyokuwa
kwao.
Tetemeko la ardhi lilitokea
mkoani Kagera mapema mwezi huu, limesababisha vifo ambapo wananchi 17
waliopoteza maisha yao, majeruhi 440 ambao walitibiwa katika vituo
mbalimbali vya afya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Pamoja na rambirambi hiyo,
Serikali pia iliwahudumia marehemu waliopoteza uhai wakati wa tukio hilo
kwa kutoa majeneza pamoja na usafiri wa kusafirisha miili ya marehemu
hao kutoka Bukoba mjini hadi kwenye maeneo ambayo familia zao walipo
ambapo yalipofanyika maziko ya wapendwa wao.
0 maoni:
Chapisha Maoni