Alhamisi, 29 Septemba 2016

PATO LA TAIFA LAONGEZEKA NA KUFIKIA TRILIONI 11.7 KWA KIPINDI CHA PILI CHA ROBO MWAKA 2016

  Posted by Esta Malibiche on Sept 29.2016 in NEWS

ver2
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akitoa taarifa ya Pato la Taifa Robo ya Pili (Aprili – Juni) ya Mwaka 2016 kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa wa Ofisi hiyo Daniel Masolwa. Taarifa hiyo imeonyesha kuwa Pato la Taifa limekua kwa kasi ya asilimia 7.9 katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2016 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 5.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

ver1
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akitoa taarifa ya Pato la Taifa Robo ya Pili (Aprili – Juni) ya Mwaka 2016 kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa ofisi hiyo Bi. Joy Sawe. Taarifa hiyo imeonyesha kuwa Pato la Taifa limekua kwa kasi ya asilimia 7.9 katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2016 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 5.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

ver3
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa (hayupo pichani) wakati akitoa taarifa ya Pato la Taifa Robo ya Pili (Aprili – Juni) ya Mwaka 2016 leo jijini Dar es Salaam. Taarifa hiyo imeonyesha kuwa Pato la Taifa limekua kwa kasi ya asilimia 7.9 katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2016 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 5.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. (PICHA NA EMMANUEL GHULA)
……………………………………………………………
Na Veronica Kazimoto-Dar es Salaam
Pato la Taifa limekua kwa jumla ya thamani ya Shilingi trilioni 11.7 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2016 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 10.9 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema ukuaji wa pato la Taifa umetokana na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, misitu na uvuvi ambapo shughuli  hizo zimekuwa  kwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

Kwa upande wa shughuli za uchumi za viwanda na ujenzi, Dkt. Chuwa alisema kumekua  na ongezeko la asilimia 20.5 katika kipindi hicho ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 11.2 mwaka 2015 katika shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto.

Aidha shughuli za uzalishaji bidhaa na viwanda zimeongeza kwa asilimia 9.1 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2016 ukilinganisha na kasi ya asilimia 5.2 ya mwaka 2015.

Shughuli za uchukuzi na uhifadhi, Dkt. Chuwa amesema kuwa shughuli hizo zimekua kwa kiwango cha asilimia 30.6 zikisababishwa  na usafirishaji wa abiria kwa njia ya reli na barabara ikiwa ni pamoja na usafiri wa UDART.

Vilevile, shughuli za fedha na bima zimeongezeka kwa kasi ya asilimia 12.5 ikilinganishwa na asilimia 10.0 iliyopatikana katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

Dkt. Chuwa amefafanua kuwa  huduma za elimu zimekua kwa kasi ya asilimia 8.0 katika robo hiyo ya mwaka ikilinganishwa na aslimia 7.4 ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2015 ambapo ukuaji wa shughuli hii imetokana na ongezeko la wanafunzi waliodahiliwa mwaka 2016.

Kwa upande wa Nchi za Afrika Mashariki ambazo zimeshachambua na kutoa Pato la Taifa katika kipindi kinachoishia Juni 2016 ni Rwanda ambapo Pato halisi la Nchi ya Rwanda katika kipindi cha Aprili – Juni 2016 limeendelea kukua kwa asilimia 5.4 ikilinganisha na asilimia 7.2 ya miezi kama hiyo mwaka 2015.
Takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka hupimwa kwa kutumia thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa nchini katika vipindi vya miezi mitatu mitatu ambavyo ni Januari – Machi, Aprili – Juni, Julai – Septemba na Oktoba – Desemba ambapo hujumuisha shughuli zote za kiuchumi, na hutumika katika kutathmini, kupanga mipango na kutayarisha sera za kiuchumi.

0 maoni:

Chapisha Maoni