Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Serikali imeendelea kupokea na kuhakiki madai ya watumishi wa umma yanayohusu mshahara na kuyalipa kadri ya uwezo wake kifedha.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Angellah Kairuki alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Singida Mjini Mhe.
Mussa Sima lililohusu mpango wa Serikali kulipa madeni ya watumishi.
Waziri Kairuki amesema kuwa
katika mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali ililipa madai ya malimbikizo ya
mshahara wa shilingi 56,293,372,627.37 ambapo yalilipwa kwa watumishi
55,688 waliokuwa na madai yatokanayo na kupandishwa vyeo, ajira mpya na
sababu nyinginezo.
Aidha, Waziri Kairuki amesema
kuwa kwa mwaka 2015/2016 Serikali imeendelea kulipa madai ya malimbikizo
ya mshahara wa watumishi wa umma ambapo hadi kufika mwezi Juni, 2016
watumishi 31,032 walilipwa jumla ya shilingi 28,929,095,373.89.
Pia ameongeza kuwa madai ya
mishahara ya watumishi 7,871 yenye jumla ya shilingi 13,754,462,429.29
yameshahakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kitumishi za
mshahara yakisubiri kulipwa na madai ya watumishi 8,776 yanaendelea
kuhakikiwa ili yaingizwe kwenye mfumo tayari kwa kulipwa.
Akijibu swali la Mhe. Zubeda
Sakuru (Viti Maalum) lililohusu changamoto ya maslahi kwa watumishi wa
sekta ya afya Waziri Kairuki amesema kuwa Serikali inatambua na
kudhamini mchango unaotolewa na madaktari, matabibu na wauguzi nchini.
Hivyo, Serikali imeendelea na
jitihada za kuboresha mishahara ya watumishi wake mwaka hadi mwaka
ikiwemo ya wataalamu wa sekta hiyo kwa kuzingatia uwezo wa Serikali wa
kulipa.
Waziri Kairuki amesema kuwa
Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi, punde
itakapokamilika itapanga mishahara na motisha upya kwa watumishi wote wa
umma wakiwemo wa sekta ya afya.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali
itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi kadri ya uwezo wake wa kulipa
utakavyoimarika ambapo katika shughuli za kila siku madeni huzalishwa
lakini ni azma yake kuhakikisha madeni hayo yanalipwa mara
yanapojitokea.
Mbali na hayo, Waziri Kairuki
ametoa wito kwa wataalamu wa afya na watumishi wote kwa ujumla kufanya
kazi kwa bidii na kwa kuzingatia viapo na maadili ya kazi zao.
0 maoni:
Chapisha Maoni