Tanzania inatarajiwa kuwa miongoni mwa nchi kumi zenye uchumi bora barani Afrika na ya kwanza kiuchumi katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki miaka ijayo kutokana na ukuaji wake mzuri wa kiuchumi, kutoagiza bidhaa za nje kwa wingi pamoja na kubana matumizi yasiyo ya lazima.
Hayo yamesemwa na Gavana Mkuu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Profesa Beno Ndulu katika makao makuu ya benki hiyo yaliyopo jijini Dar es Salaam na kusema kuwa shughuli zitakazochangia ukuaji wa uchumi kwa kasi ni pamoja na uzalishaji umeme kwa kutumia gesi, uzalishaji saruji, mauzo ya bidhaa za ndani nje ya nchi, shughuli za viwandani na makusanyo ya kodi.
Amesema katika kipindi cha robo ya Mwaka 2016 ukuaji wa pato la taifa unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.7 katika kipindi kama hicho Mwaka 2015. “Hali ya ukuaji uchumi Tanzania bado ni nzuri na kwa matarajio ya miaka ijayo itakuwa miongoni mwa nchi kumi zenye uchumi imara barani Afrika, pia itakuwa nafasi ya kwanza katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema.
Profesa Ndulu ameeleza kuwa sekta za fedha, mawasiliano na utawala wa umma zimekuwa kwa kasi katika kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka 2016 na kwamba inadhihirisha kuwa uchumi wa nchi utaendelea kuimarika kwa mwaka huu. “Kilimo kimechangia kwa asilimia 11.7, biashara 10.6, uchukuzi 10.1, fedha 10.1 na mawasiliano asilimia 10,” amesema.
Ameeleza kuwa “Kwa upande wa matumizi ya serikali kiujumla na bajeti, juhudi zilizofanyika kwa upande wa kuongeza mapato na kudhibiti matumizi imesaidia bajeti kutekelezwa bila ya athari. Kuanzia Januari hadi Juni MMwaka huu misaada halisi iliyotumika ni asilimia 1 na mikopo ni asilimia 8, asilimia 91 ya bajeti ni ya mapato na mikopo ya ndani, hatukuwa na hali hii kwa muda mrefu, hivyo ni hatua nzuri iliyofikiwa na serikali,”
Prof. Ndulu amesema shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa tulivu kutokana na BOT kusimamia vizuri hali ya ukwasi kwenye uchumi pamoja na mwenendo wa uchumi ndani na nje ya nchi.
“Kwenye upande wa mwenendo wa thamani ya shilingi katika kipindi cha mwaka mzima mwenendo wa thamani ya shilingi uko tulivu na siku za hivi karibuni umeimarika kidogo na matarajio yetu shilingi iendelee kuwa tulivu kwa sababu ukuaji wa mauzo nje umeendelea kuwa vizuri,” amesema na kuongeza.
“Sababu iliyopelekea shilingi kuwa imara ni pamoja na katika kipindi cha nusu mwaka wa kwanza mauzo ya bidhaa za nje yamekuwa kwa asilimia 14.2, kupungua kuagiza kwa bidhaa za nje holela, kupunguza matumizi ya mafuta katika kutengeneza umeme na viwandani sasa inatumika gesi, hali hii imepunguza kuagizwa vitu nje.”
Pia amesema licha ya mikopo na misaada kupungua hakujaathiri bajeti ya nchi. “Kupungua mikopo hiyo hakumaanishi kuwa tunanyimwa mikopo bali tunaikwepa sababu sasa inamasharti magumu ,wenzetu waliochukua mikopo sasa wako katika wakati mgumu kwa sababu masharti yake ni magumu,” amesema.
Ameongeza kuwa “Mapato yetu ya fedha za kigeni na matumizi pengo lake limepungua kwa asilimia 61, unapoagiza vitu na kukopa nje kunaathiri uchumi. Uchumi wetu utasimama imara kwa sababu karibu sehemu kubwa ya kile tunachoagiza tunatumia shilingi yetu wenyewe. Pia akiba ya fedha za kigeni bado nzuri tuna dola bilioni 4 za kimarekani zenye uwezo uwezo wa kununua bidhaa katika kipindi cha miaka minne mfululizo,”