Posted by Esta Malibiche on Sept25.2016 in NEWS
Hussein Makame-NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
imewaomba wakerugenzi na wenyeviti wa halmashauri nchini kuwapa ridhaa
watendaji na makamishna wa Tume hiyo watakaofika katika maeneo yao ili
kutoa elimu ya mpigakura kwenye maeneo yao.
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani wakati akiwasilisha mada kwenye
Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT)
uliomalizika mwishoni mwa wiki hii mjini Musoma mkoani Mara.
Bw. Kailima aliomba iwapo maafisa uchaguzi au mtendaji na
makamishna wa tume watafika maeneo yao wawape fursa ya kukutana na
mabaraza ya madiwani na mikutano ya vijiji na mitaa na kukutana na
watendaji wengine ili kutoa elimu ya mpiga kura.
“Kwa hiyo niwaombe waheshimiwa wenyeviti na wakurugenzi, wale
watendaji maafisa uchaguzi kwenye halmashauri zenu au mtendaj na
makamishna wa tume wanapofika pale muwape fursa ya kukutana na mabaraza
ya madiwani”, alisema Bw. Kailima na kuongeza kuwa:
“Niwaombe muwape fursa ya kwenda kwenye mkutano Mkuu wa kijiji
au mkutano mkuu wa mtaa, kuwapa fursa ya kukutana na watendaji wengine
kwenye eneo lako au kwenye shule za sekondari.Tunaomba muwape ridhaa ya
kwenda kutoa elimu hiyo na tunaomba Mungu atuongoze ikifika mwaka 2019
asiwepo mtendaj
ambaye hajui tume angalau majukumu yake.”
Alisema lengo la kuwepo kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwenye
mkutano huo ni kutoa elimu ya mpiga kura na ambalo nii jukumu la
Kikatiba la Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Ukisoma ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuru ya Muungano wa
Tanzania ibara ndogo (6) (e) inasema Tume itatekeleza majukumu mengine
yote kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge” alifafanua Bw. Kailima
na kusisitiza kuwa:
“Ukisoma pia kifungu cha 4 C cha Sheria ya Uchaguzi, Tume
inaelekezwa Kutoa elimu ya mpiga kura nchini nzima na kusimamia na
Kuratibu Asasi na Taasisi zinazotoa elimu hiyo.”
Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi alibainisha kuwa uzoefu unaonesha
kuwa elimu ya mpiga kura imekuwa ikitolewa wakati wa kipindi cha
Uchaguzi Mkuu tu na hata hivyo maeneo mengi yanashindwa kufikika.
Alisema madiwani ambao walihudhuria mkutano huo wa ALAT ni
wenyeviti wa kamati za maendeleo ya Kata hivyo iwapo diwani akishiba
elimu ya mpiga kura atahamasisha elimu hiyo kwa wenyeviti wa vijiji na
hatimaye kuhamasisha elimu hiyo ifike hadi kwa wanavijiji.
NEC imeweka mikakati mbalimbali ya kutoa elimu ya mpiga kura
ambapo katika mkutano huo mbali na kutoa elimu kwa wajumbe wa mkutano
huo lakini pia ilitoa elimu hiyo kwenye shule ya Sekondari ya Songe ya
mjini Musoma na kukutana na wananchi kuwapa elimu hiyo kwenye maonesho
ya mkutano huo.
0 maoni:
Chapisha Maoni