Meneja wa Mradi wa Uwezeshaji
Vijana Kiuchumi (YEE) – Tanzania, Simon Ndembeka akiongea na waandishi
wa habari (hawapo pichani) kuhusu uhitaji wa walimu wa mahitaji maaalum
watakaoweza kukidhi idadi ya wanafunzi walemavu wanaohitaji kupatiwa
elimu ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Ufundi Stadi (VETA) chini ya
mradi huo.
Baadhi ya Vijana waliohitimu
katika fani ya ufundi wa magari chini ya Mradi wa Uwezeshaji Vijana
Kiuchumi (YEE) wakifanya mazoezi ya kurekebisha magari katika gereji ya
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, (mwenye tisheti jekundu) ni fundi
msaidizi wa gereji hiyo, Haji Faki.
……………………………………………………….
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Kisarawe
Shirika lisilokuwa la kiserikali
la Plan International wameishauri Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
(VETA) kuongeza walimu waliobobea katika ufundishaji wa wanafunzi
walemavu ili kuhakikisha wanapata elimu sawa na wengine.
Ushauri huo umetolewa na Meneja
wa Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) – Tanzania, Simon Ndembeka
baada ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum
wanaohitaji kupatiwa elimu ya ufundi katika vyuo hivyo.
Meneja Mradi amesema kuwa
nyakati za kuwaficha walemavu majumbani zimekwisha na kwa sasa wazazi
wanafahamu kuwa ulemavu sio mwisho wa maisha hivyo muamko wa walemavu
wanaohitaji kusoma umekuwa mkubwa tofauti na zamani.
“Mradi huu umetenga asilimia 10
kwa ajili ya jamii ya vijana wenye ulemavu kupatiwa mafunzo ya ufundi
katika chuo cha VETA ili baadae waweze kuendesha maisha yao lakini lengo
hilo lina changamoto kubwa ya upungufu wa walimu wa taaluma hiyo hivyo,
tunaishauri VETA kuongeza walimu wa aina hiyo ili kukidhi uhitaji wa
idadi ya wanafunzi walemavu”, alisema Ndembeka.
Ndembeka ameongeza kuwa kitendo
cha kuwawezesha vijana wenye ulemavu ni moja ya lengo la mradi huo kwani
kundi hilo ndilo kundi lenye changamoto nyingi za kimaisha kuliko kundi
lingine lolote hivyo kuwapatia elimu kutawasaidia kuweza kupata ajira
au kujiajiri na hatimaye kuweza kuyakomboa maisha yao.
Aidha, Ndembeka ameishukuru
Serikali kwa ushirikiano wao wa kutoa misaada ya mikopo, elimu, maeneo
ya vijana kufanyia mazoezi pamoja na ushiriki wao kama wageni rasmi
katika mahafali mbalimbali za vijana wanaohitimu elimu ya ufundi chini
ya mradi huo.
Kuhusu suala la kuwasaidia
vijana kupata ajira amefafanua kuwa mara nyingi wamekuwa wakifanya vikao
na waajiri wa sekta mbalimbali nchini ili kuwajengea ufahamu waajiri
juu ya uwepo wa vijana hao pamoja na kujadili jinsi ya kuwasaidia kwa
kuwapatia ajira.
Mradi huo wa miaka mitatu
unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI,
CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la
Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
0 maoni:
Chapisha Maoni