Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Singida, kimewatumbua wapangaji wake 15 kwenye vibanda vya biashara kwa tuhuma ya kuhujumu mapato ya chama hicho tawala.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake juzi,katibu CCM manispaa ya Singida, Charles Charles, alisema wafanyabishara hao waliokuwa wamepanga kwenye vibanda vilivyopo eneo la Msufini, wameondolewa baada ya kukiuka mikataba waliyowekeana na CCM.
Akifafanua,alisema wafanyabishara hao walikiuka mikataba kwa kupangisha wafanyabiashara wengine na kuwatoza kodi kubwa zaidi ya ile iliyoelekezwa na CCM manispaa ya Singida.
“Hawa wafanyabishara waligeuza miradi ya CCM manispaa ya Singida,kuwa ni ‘shamba la bibi’.Kwenye baadhi ya mikataba walioyowekeana na ofisi yangu,walitakiwa kulipa shilingi 40,000 kwa mwezi, lakini wao wakavunja mkataba, kwanza kwa kupangisha wafanyabishara wengine,pili wakawa wanawatoza kodi mara tatu ya bei iliyopo kwenye mikataba,” alifafanua Charles.
img_8163Katibu CCM manispaa ya Singida,Charles Charles, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo picha) juu ya kuwafukuza wafanyabiashara 15 wapangaji wa vibanda katika eneo la Msufini mjini hapa.Wafanyabiashara hao wamefukuzwa baada ya kukiuka mikataba yao.(Picha na Nathaniel Limu)
Akifafanua zaidi, katibu huyo alisema kitendo hicho walichofanya wafanyabishara hao, kimekuwa kikiingiza hasara ya zaidi ya shilingi laki sita kwa mwezi.
“Wapangaji hawa wamevunja mikataba kwa makusudi …. kipengere cha tatu cha mikataba kifungu kidogo cha (h) kinachosema mpangaji ‘hatatoa au kupangisha au kukondisha na kuongeza eneo lililopangishwa bila idhini ya maandishi kutoka kwa mpangishaji,” alisema.
Katibu Charles alisema baada ya kuwaondoa wapangaji hao,vibanda hivyo vya biashara sasa vitakuwa vimepangwa na wafanyabiashara waliowekwa na wapangaji wa awali waliokuwa wamewekeana mikataba na CCM,halafu wakafanya mambo kinyume na mikataba.
“Hata hivyo, tunawashukru wapangaji waliovunja mikataba yao na CCM manispaa ya Singida, kwa kutupatia wapangaji wanaolipa kodi kubwa zaidi.Hawa sasa tutaingia nao mikataba mipya ya upangishaji,” alisema.
Katika hatua nyingine,katibu huyo alisema ‘operation’ ya kukagua vibanda 77 vya miradi ya biashara, inaendelea ili kubaini wapangaji wanaokwenda kinyume na mikataba yao.
Akisisitiza,alisema CCM wanaispaa ya Singida, inajipanga upya kuhakikisha miradi yake inaingiza pato la kukidhi mahitaji halisi ya chama na kuondokana na tabia ya ombaomba.
Na Nathaniel Limu, Singida