Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akizungumza na waandishi wa habari leo.
Shule za Ihungo na Nyakato zikivunjwa tayari kwa ujenzi mpya.
……………………………………………………………..
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba.
Serikali imesema gharama za
kujenga upya wa shule za sekondari za Ihungo na Nyakato ni Sh. Bilioni
60 hadi kukamilika kwa miundombinu yake ambayo itakayoruhusu wanafunzi
kupata elimu kama kawaida.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu leo mjini Bukoba alipokuwa
akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na
Serikali katika kukabiliana na athari zilizosababishwa na tetemeko la
ardhi lililoukumba mkoa huo.
Katika kukamilisha ujenzi wa
shule hizo, Mkuu wa mkoa amesema kuwa hatua ya kuvunja wa majengo yote
imeshaanza ambapo tayari Kampuni ya CHICO ya Wachina inaendelea na
uvunjaji wa majengo yote ili kazi ya ujenzi uanze..
“Wataalam wote wa ujenzi kutoka
idara mbalimbali za Serikali wanaendelea na uchambuzi yakinifu wa
majengo mapya ya shule hizo utakaozingatia viwango vya ujenzi ambapo
ghrama za awali kwa tathmini iliyotolewa na wataalamu hao ni Sh. milioni
30 kwa shule za Ihungo na Nyakato” alisema Meja Kijuu.
Uamuzi wa kuzijenga shule hizo
upya zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi, ulipelekea Serikali kuzifunga
na kuwahamisha wanafunzi waliokuwa wanasomea katika shule za Sekondari
Ihungo na Nyakato ili waweze kuendelea na masomo wakati shule zao
zinajengwa upya.
Wanafunzi wa shule hizo tayari
wamepangiwa shule watakazoenda ili kuendelea na masomo kulinhgana na
mihula ya mwaka na ratiba za vipindi vya masomo kila siku.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amesema
kuwa katika kuhakikisha ujenzi wa majengo ya taasisi za Serikali na
wananchi yanakuwa imara na salama, wataalam wa Wakala wa Jiolojia
Tanzania ndio watatoa ushauri wao kabla ya ujenzi mpya haujaanza ili
ujenzi wa majengo mapya ufanyike sehemu sahihi.
Kuhusu misaada inayotolewa na
Serikali, nchi rafiki, wadau na wananchi, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa
Kamati ya Maafa katika kukabiliana na athari za tetemeko kwa wananchi
walioathirika tayari imetoa mahitaji mbalimbali kwa waathirika wa
tetemeko hilo.
Mahitaji yaliyotolewa kwa
wananchi ni pamoja na unga wa sembe kilo 3,450, sukari mifuko 410,
mchele kilo 3,150, maharage kilo 5,753, maji katoni 850, sabuni katoni
24, mashuka 90, mablanketi ya watu wazima na watoto 2,020, vyandarua
1,274, sare za wananfunzi 570, magodoro 694, mahema 127 na matrubali
2,760.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa
amezitaka Kamati za Maafa za Wilaya zikarabati miundombinu ya kutolea
huduma za kijamii ikiwemo shule za sekondari na msingi, vituo vya
kutolea huduma za afya vilivyoharibiwa na tetemeko la ardhi ili huduma
hizo muhimu ziweze kurejea mara moja na kutoa huduma kwa wananchi.
Hadi sasa wamebaki jumla ya
majeruhi 13 ambapo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamebakia majeruhi
tisa, Hospitali ya Mugana majeruhi wawili na Hospitali ya Rufaa ya
Bugando majeruhi wawili ambao wanaendelea kupata huduma za matibabu na
hali zao zinaendelea vizuri.
Tetemeko la ardhi lililotokea
Septemba 10, 2016 Mkoani Kagera lilisababisha vifo vya watu 17, majeruhi
440, majeruhi 427 tayari wametibiwa na kuruhusiwa katika Hospitali ya
Rufaa ya mkoa na vituo mbalibali vya afya kwenye mkoa.
0 maoni:
Chapisha Maoni