Posted by Esta Malibiche on Sept29.2016 in NEWS
Na mwandishi wetu
Tatizo lolote linapotokea katika
jamii huambatana na mambo mbalimbali ikiwemo kutembelewa na wageni
wakiwemo waandishi wa habari.
Hali hiyo imetokea katika
Manispaa ya Bukoba kufuatia tetemeko la ardhi lililoathiri mkoa huo
pamoja na miundombinu mbalimbali ambapo shule ya msingi Kashai nayo
ilipata athari za tetemeko hilo.
Athari hiyo ya tetemeko
ilipelekea chombo kimoja cha habari cha televisheni nchini kuripoti
katika taarifa ya habari kuwa shule hiyo imefungwa na wanafunzi
wamerudishwa nyumbani mara baada ya kumaliza likizo fupi badala ya
kuendelea na masomo.
Taarifa ya kufungwa kwa shule
hiyo inakanushwa na aliyekuwa Mwalim Mkuu wa Shule ya Msingi Kashai,
Gideon Kenjori Akizungumzia kuhusu suala hilo na kusema kuwa shule
haijafungwa na wanafunzi wanaendelea kusoma kama kawaida.
Mwalimu huyo amesema kuwa habari
hiyo iliyotangazwa haikuwa na ukweli wowote kwa kuwa wanafunzi
wanaendelea na masomo kwa madarasa yote huku akimshangaa mwandishi wa
habari aliyetoa habari hiyo na kusema alijitengenezea habari aliyeitaka
yeye na sio hali halisi ya shule ya Kashai.
“Shule haijafungwa, mimi sikuja
na mwandishi wala sikuwepo,mwandishi alikurupuka na kuenda nyuma na wala
hakuja ofisini na hajaonana na sisi, yeye aliripoti ya kwake aliyeyaona
na hakuna mtu ambaye aliongea nae, aliandika ya kwake na amepata
taarifa alizotaka alikojua” alisema Mwalimu Gideon.
Mwalimu huyo amesema kuwa athari
za tetemeko limeharibu vyumba saba vya madarasa ambavyo havifai
kutumika, vyumba nane vinaweza kutumika na nyumba ya mwalimu imepata
nyufa hatarishi.
Ili kuhakikisha wanafunzi wote
wanasoma umefanyika utaratibu wa wanafunzi kusoma kwa awamu ambao ni
wanafunzi wa darasa la kwanza na pili na wanafunzi wengine wa darasa la
tano na la sita wamehamishiwa katika shule ya msingi Tumaini ambapo kuna
madarasa manne yaliyowazi wakati wanafunzi wa madarasa mengine
yaliyobaki wanaendelea na masomo shuleni hapo.
Mwl. Gideon ameongeza kuwa uwezo
wa kufunga shule haupo chini ya Mwalimu Mkuu bali mamlaka ya kufunga
shule inatoka kwa uongozi wa juu ambao ndio wenye uwezo huo, kwa maana
hiyo shule haikufungwa.
Katika kuhakikisha wanafunzi
wanaendelea na masomo kulingana na ratiba ya muhula wa masomo, Uongozi
wa Manispaa ya Bukoba umeagiza walimu ambao nyumba zao hazifai kutumika
watafute nyumba za kupanga na manispaa italipia gharama za nyumba hizo
wakati utaratibua kukarabati au kujenga nyumba zao unaendelea ili
maisha yao yaendelee kama kawaida waweze kutimiza majukumu yao ya
kufundisha.
0 maoni:
Chapisha Maoni