Posted by Esta Malibiche on Sept29.2016 in NEWS
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ametoa mwezi mmoja kwa watumishi waliohamishiwa wilaya mpya ya Kibiti
mkoani Pwani kuripoti katika kituo chao cha kazi na watakaoshindwa
kutekeleza watakuwa wamejifukuzisha kazi.
Amesema mtumishi yeyote
aliyehamishiwa wilaya hiyo ambaye anaishi nje ya Kibiti anatakiwa arudi
na kuishi kwenye makao makuu ya wilaya na si vinginevyo.
“Tayari nimemuagiza ndugu Zuberi
Samatabu Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani kuhakikisha anasimamia
watumishi wote wa wilaya hiyo wanaoishi nje ya wilaya hiyo waishi
Kibiti na si Ikwiriri,” amesema.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu
ilifuatia taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo
Alvera Ndabagoye ambaye alimueleza Waziri Mkuu kuwa ni watumishi wanane
pekee kati ya 74 waliopangiwa kufanya kazi kwenye wilaya hiyo
wameripoti katika kituo cha kazi
Ili kukabiliana na tatizo la
uhaba wa nyumba za watumishi amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi
Evarist Ndikilo kuzungumza na watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii
kwenda wilayani huko kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa nyumba za
watumishi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo (Jumatano, Septemba 28, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa
wilaya hiyo katika ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo,utendaji
wa serikali na kutoa msimamo wa serikali kuhusu utekelezaji wa majukumu
yake ya kila siku
Wakati huo huo Waziri Mkuu
amewataka madiwani wa halmashauri hiyo wawe wakali katika kusimamia
miradi ya maendeleo na kuacha tabia ya kuomba omba kwa wakuu wa idara
ili kuepuka kujishushia hadhi zao na kupelekea kuhujumiwa kwa miradi
mbalimbali ya jamii
Aidha aliwataka viongozi wa
wilaya hiyo kutengeneza mazingira ya kukaribisha wawekezaji na
wahakikishe kwamba uwekezaji utakaofanyika hausababishi migogoro ya
ardhi kwa wananchi
Waziri Mkuu amewahamasisha
wananchi kuhakikisha wanapeleka watoto shule kwa maana Serikali imebeba
mzigo wote wa gharama za ada na uendeshaji wa shule hizo. Alisisitiza
kuwa njia pekee na ya haraka kuondoa umaskini ni kusomesha watoto
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
ameagiza halmashauri zote nchini kutumia mfumo wa kieletroniki katika
ukasanyaji wa mapoto ili kuziba mianya ya uvujaji mapato haswa ya
maliasili
0 maoni:
Chapisha Maoni