Na. Abushehe Nondo na Immaculate Makilika- MAELEZO
Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed
Chande Othman amesema kuwa Serikali inatarajia kuzindua mpango mkakati
wa Mahakama ya Tanzania kwa miaka 5 unaolenga kuboresha huduma za
kimahakama nchini.
Aidha Jaji Mkuu alisema uzinduzi
wa mpango huo utaenda sambamba na mradi wa maboresho wa huduma za utoaji
haki nchini uliogharimu kiasi cha Tsh Bilioni 140.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam Jaji Chande alisema kuwa mradi huo una nguzo
tatu ambazo ni utawala bora na uwajibikaji , fursa ya kutoa na kupata
haki na uharakishaji wa mashahuri ambapo kwa pamoja umekusudia kutoa
haki kwa wote na kwa wakati.
“Katika kujenga imani ya wananchi
kwa mahakama tunataka kufikia sehemu ambapo mtu yeyote akileta shauri
lake Mahakamani basi litasikilizwa kwa wakati” alisema Jaji Chande.
Aliongeza kuwa taarifa za hivi
karibuni zinaonyesha kuwa asilimia 47 ya Watanzania hawana fursa sawa ya
kupata haki ya Mahakama katika maeneo waliopo hususani mikoani kwa kuwa
mikoa mingi haina Mahakama Kuu, hivyo mpango huo utakaozinduliwa
utalenga kuboresha utendaji na utoaji huduma za kimahakama nchini.
Akizungumzia kuhusu mradi wa
maboresho ya huduma za Mahakama ambao unaandaliwa kwa ushirikiano wa
Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia Jaji Chande alisema kuwa mradi
huo unalenga kuimarisha mifumo ndani ya Mahakama, kuendesha kesi na
utoaji wa hukumu kwa wakati.
Jaji Chande aliongeza kuwa mradi
huo utapanua wigo wa utoaji huduma za kimahakama ambapo itatoa fursa za
mafunzo endelevu kwa watumishi wa Mahakama 6400 wa ngazi mbalimbali.
Aidha alisema mpango huo utasaidia
kuimarisha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kukijingea
uwezo wa kutoa taaluma bora kwa watumishi pamoja na wadau katika masuala
ya Sheria.
Jaji Chande alisema tayari mradi
huo umewezesha kujengwa kwa Mahakama tano za kisasa zilizopo katika
maeneo ya Kibaha, Kawe, Kisarawe, Kigamboni na Bagamoyo ambazo zitakuwa
mfano wa uanzishwaji wa Mahakama za kisasa nchini.
Mradi huo unaogharimu bilioni 140
utazinduliwa Kibaha mkoani Pwani Septemba 21 mwaka huu, ambapo mgeni
rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni