Posted by Esta Malibiche on Sept30.2016 in NEWS
Grace Singida.
Wizara ya afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee imeishauri mikoa yote ya Tanzania bara
kuiga mfano wa mkoa wa Singida wa kuanzisha huduma za kibingwa za mkoba
kwa ngazi za wilaya ili kuwafikia watanzania wengi wenye uhitaji.
Mkurugenzi wa tiba kutoka wizara
hiyo Dokta Magreth Mhando ametoa ushauri huo katika hospitali ya
Mtakatifu Calorus Mtinko Singida Vijijini alipotembelea kujionea awamu
ya pili ya zoezi la huduma za kibingwa za Mkoba.
Dokta Mhando amesema kumekuwa na
huduma za kibingwa za mkoba ila hazikufanyika vizuri kama ambavyo mkoa
wa Singida umekuwa ukifanya na kutoa pongezi za Wizara kwa Mkuu wa mkoa
na Mganga mkuu wa mkoa kwa ubunifu huo.
Amesema huduma za kibingwa za
mkoba zimekuwa zikiratibiwa na taasisi au hospital kubwa kama Muhimbili
ambapo madaktari bingwa wamekuwa wakitoa huduma kwa ugonjwa fulani na
kwa ngazi ya hospitali za Mkoa tofauti na zoezi linaloendelea Mkoani
Singida la kutoa huduma za kibingwa kwa magonjwa mbalimbali.
Dokta Mhando ameongeza kuwa
kutokana na uhaba wa madaktari bingwa nchini wizara imetenga fedha kwa
ajili ya kuwasomesha madaktari na kuwashauri waajiri ambao ni makatibu
tawala wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya
kuwasomesha madaktari hao kwakwuwa wizara pekee haitaweza.
Amesema utaratibu ni kuwa na
madaktri bingwa angalau watano kila Mkoa lakini mikoa mingi haina idadi
hiyo huku akiongeza kuwa lengo la kutembelea zoezi hilo Singida
nikujionea hali halisi na sio kusubiria taarifa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi
Mathew John Mtigumwe mara baada ya kutembelea wodi zote na kuzungumza na
wagonjwa waliopata huduma za kibingwa amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa
kuongeza muda wa kutoa huduma hiyo kutoka siku tano hadi nane kutokana
na wingi wa wagonjwa waliojitokeza.
Mhandisi Mtigumwe amesema huduma
hiyo inasaidia kutambua magonjwa na kuyatibu kabla hayajawa sugu lakini
pia gharama zikiwa nafuu kutokana na kusogezwa kwa ngazi za halmashauri.
Ameongeza kuwa lengo la ofisi
yake ni kuhakikisha huduma za kibingwa za mkoba zinapelekwa kwa kila
halmashauri na endapo zoezi likikamilika na kukiwa na uhitaji mkubwa
kuna uwezekano mkubwa wa kurudia zoezi hilo.
Mhandisi Mtigumwe amesema
kuelekea Tanzania ya viwanda afya bora ni muhimu na wazalishaji wakubwa
ni wananchi wa ngazi za chini hivyo huduma hiyo itasaidia kuimarisha
afya ili waweze kuzalisha bidhaa kwa wingi na zenye ubora.
Amesema kwa wale wagonjwa
watakaopewa rufaa kwenda nje ya Mkoa utaratibu utaangalia wa kuwapatia
usafiri wa Mkoa ili kuwapeleka hasa wale wasiojiweza.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta
John Mwombeki amesema kwa muda wa siku tano wagonjwa zaidi ya 800
wameonana na madaktari bingwa huku idadi ikitarajiwa kuongezeka kutokana
nakuongezwa kwa siku za klutoa huduma.
Dokta Mwombeki amesema wagonjwa
wengi wanaofika wanatoka maeneo mbalimbali hasa maeneo ya kijijini na
wenye hali duni ya maisha hivyo zoezi hilo limesaidia wananchi hasa
wwenye kipato cha chini.
Amesema madaktari bingwa wanaotoa
huduma za kibingwa za mkoba ni madaktari bingwa wa magonjwa ya akina
mama, watoto, macho, meno, magonjwa ya ndani na daktari bingwa wa
upasuaji.
Wagonjwa waliopata huduma
wameushukuru uongozi wa mkoa kwa kubuni utaratibu wa kuwafuata wagonjwa
karibu ili kuwapatia huduma za kibingwa kwakuwa inawasaidia kupata
matibabu mapema kabla magonjwa hayajawa sugu na kushauri huduma iwe
endelevu angalau kila mwaka.
0 maoni:
Chapisha Maoni