Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J.
Kairuki (Mb) akiongea na vyombo vya habari kuhusu masuala ya Utumishi wa
Umma nchini Tanzania hivi karibuni. (Picha ya Maktaba).
……………………………………………………………………………………………
Makala iliyopita Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) aliongea kuhusu matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini, pamoja, Matumizi ya Nyaraka
za Serikali na Maadili kwa viongozi kwa viongozi wa Umma. Waziri Kairuki
aliongea hayo katika Runinga ya Taifa (TBC), makala ya leo ni sehemu ya
mwisho na inaangalia mapambano dhidi ya rushwa na mpango wa kunusuru
kaya masikini hapa nchini.
Mapambano dhidi ya rushwa
Waziri Kairuki alieleza Serikali
imekuwa ikichukua hatua katika kuzuia na kupambana na rushwa nchini
mfano kwa kufuatilia fedha za Miradi ya Maendeleo kupitia Ofisi za Kanda
za TAKUKURU kwa lengo la kuhakikisha thamani ya miradi inayotekelezwa
inaendana na kiasi cha fedha kilichotolewa ambapo ufuatiliaji huo
umeiwezesha Serikali kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 39.34.
“Tumewasilisha majalada 297 kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa ajili ya kuombewa kibali cha
mashitaka ambapo majalada 229 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa
mahakamani” Waziri Kairuki alifafanua.
Aliongeza mikakati ya serikali ni
pamoja na kuhuisha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Na. 11 ya 2007
ili kujumuisha makosa ya uhujumu uchumi na kutaifisha mali zilizopatika
na kwa njia ya Rushwa na Ufisadi.
Kuhusu kaya masikini hali ikoje?
Waziri Kairuki alisema Mpango wa
Kunusuru Kaya Masikini ambao utachukua miaka kumi unatekelezwa katika
Halmashauri zote za Tanzania Bara pamoja na Zanzibar.
“Katika kipindi cha miaka minne
mpango umetekelezwa Vijiji, Mitaa na Shehia 9,960 ambayo ni sawa na
wastani wa asilimia 70. Kaya 1,358,268 zimetambuliwa ambapo kati ya
hizo, Kaya 1,110,377 zimeandikishwa” Waziri Kairuki alisena na kuongeza
kaya 1,110,377 zimehawilishiwa fedha kwa kulipwa ruzuku katika awamu 16
ili kuziwezesha kuwekeza katika lishe, afya na elimu.
Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi unatekelezeka?
Waziri Kairuki alisema Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership)
ulianza kutekelezwa nchini toka mwaka 2012/13, na umejikita katika
kuweka uwazi zaidi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali;
Ushirikishwaji wa Sekta za Umma na Binafsi katika utekelezaji wa Mpango;
Uwajibikaji wa Serikali kwa Wananchi; Matumizi ya Teknolojia na
Ubunifu; na Mapambano dhidi ya Rushwa.
Alisema miongoni mwa yaliyofanyika ni pamoja na kuongezeka kwa uwazi kuhusu bajeti ya Serikali kwa kuandaa kijitabu cha “Citizen budget”
kilichoandaliwa kwa Kiswahili na lugha rahisi kwa kuchapishwa kwenye
tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango. Pia, taarifa za utekelezaji za
sekta za kipaumbele Afya, Elimu na Maji kuchapishwa katika Tovuti za
sekta hizo na kukamilika kwa zoezi la upembuzi yakinifu wa Takwimu Huria
(Open Data) ili kuongeza uwazi wa takwimu na taarifa mbalimbali;
Waziri Kairuki alisisitiza kuwa
Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za
Serikali kwa Uwazi kwa mikakati mbalimbali ikiwamo, kuendelea na
utekelezaji wa kuwa na uwazi katika bajeti ya Serikali kwa kuweka
taarifa za bajeti kwenye tovuti mbalimbali kwa lugha nyepesi na kwa
Kiswahili na kuimarisha mfumo wa Takwimu Huria ambayo utarahisha wadau
mbalimbali kupata takwimu zinazohusu masuala mbalimbali hususan Afya, na
Elimu.
Majukumu ya Ofisi ni yapi?
Ofisi ya Rais – Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) ina majukumu ya kuandaa na
kusimamia utekelezaji wa Sera za Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika
Utumishi wa Umma; Taratibu, Miundo na Mifumo ya Utoaji Huduma;
Uendelezaji Rasilimaliwatu; Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka katika
Utumishi wa Umma. Aidha, Ofisi hii inasimamia maadili ya Watumishi na
viongozi wa Umma; mapambano dhidi ya rushwa; Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii; Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge; Mfuko
wa Rais wa Kujitegemea; na Taasisi ya Uongozi.
0 maoni:
Chapisha Maoni