Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Serikali imesema imejipanga
kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi inayotokana na wathamini
kutozingatia maadili ya uthamini pamoja na kazi za uthamini kufanywa na
watu wasiokuwa na sifa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Willium Lukuvi leo mjini Dodoma
alipokuwa akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa
Wathamini mwaka 2016 katika mkutano wa nne wa kikao cha tatu cha Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Lukuvi amesema kuwa lengo
kuu la Muswada huo ni kutunga Sheria itakayoweza kusimamia taaluma na
shughuli za uthamini Tanzania Bara kwa kupunguza changamoto mbalimbali
zinazoikabili jamii na sekta ya ardhi kwa ujumla.
Aidha, Waziri huyo amesema kuwa
sheria hiyo iliyopendekezwa itasaidia katika kuwaondolea mateso wananchi
wanaothaminiwa mali zao na kuchelewa kulipwa fidia kwa kuweka ukomo wa
muda ambao fidia hiyo lazima ilipwe na kuwadhibiti wawekezaji kulipa
fidia kwa wakati.
Pia ameongeza kuwa sharia hiyo
itasaidia kuondoa utapeli uliokuwa unafanywa na wathamini kuongeza
thamani kinyume na utaratibu na kuongeza wafidiwa hewa sambamba na
kuthibiti uthamini wa kifisadi ambao umekuwa ukifanywa na wathamini kwa
kushusha thamani ya mali kwa madhumuni ya kukwepa kulipa kodi.
Zaidi ya hayo, katika usajili wa
wathamini chini ya sheria hiyo inayopendekezwa, kutakuwa na mfumo wa
kuwawajibisha wathamini ambao watakaokiuka maadili ya kitaaluma, kutoa
adhabu kwa wathamini wanaokiuka sharia hiyo ikiwa ni pamoja na kifungo,
faini kali na kusimamishwa au kufutiwa usajili.
Kwa upande wake Waziri Kivuli
kambi ya upinzani katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mhe. Wilfred Lwakatare amesema kuwa sheria hiyo ikitekelezwa itasaidia
kupunguza changamoto katika sekta ya ardhi na nyumba zilizokuwa
zinatokana na matatizo ya uthamini.
0 maoni:
Chapisha Maoni