Hospitali ya Benjamini Mkapa ya UDOM mjini Dodoma imeanza kutoa huduma ya matibabu ya ugonjwa wa Saratani kwa watoto wadogo kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Marafiki wa Watoto wanaoishi na saratani nchini – ‘friends of children with cancer’.
Mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma Dokta James Charles amewaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa hosptali hiyo itatoa huduma ya kutibu ugonjwa wa Saratani kwa wakazi wa Dodoma na mikoa ya kanda ya kati.
“Kama mnavyofahamu katika mkoa wa Dodoma tunayo hospitali ya Benjamin Mkapa na hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambayo imeongezewa uwezo mkubwa na tutaanza kutibu ugonjwa wa Saratani hususani katika kituo cha Benjamin Mkapa” amesema Dk.James
Dk James ameongeza kuwa huduma hiyo itatoa fursa kwa wakazi wa Dodoma na mikoa ya kanda ya kati kupata huduma kwa wakati bila kukaa mda mrefu wakusubiri matibabu.
Mkurugenzi wa shirika la ‘Friends of Children with Cancer’ Janet Maloni na Makamu wa Rais wa Shirika hilo wameelezea takwimu na uzoefu wao kuhusu hali halisi ya ugonjwa saratani kwa watoto nchin.
“Tafiti zinaonyesha kwamba Tanzania tunatarajia watu wanaopata saratani kwa mwaka si chini ya watu 40,000 na kati ya hao 27,000 watapoteza maisha bila kufika katika vituo vya afya” amesema Bi Janet
“Kwa watoto tunatarajia watoto 2500 wanazaliwa na tatizo hili na wanaofika katika vituo vya afya, kwa mfani kile cha Muhimbili sio zaidi ya watoto 500” ameongeza Janet
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa mkoa wa Dodoma Bw. James Charles amesema kuwa ugonjwa wa saratani kwa watoto unatibika endapo mtoto atapatiwa huduma na tiba sahihi mapema katika kituo husika cha matibabu ya saratani.
Na Hashim Ibrahim (UDSM-SJMC)