Shirikisho la Kimataifa la Mpira
wa Miguu (FIFA), kwa mara nyingine, limeagiza klabu tisa za Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Klabu sita za Ligi Daraja la Kwanza ya
StarTimes (TFDL) kujiunga mara moja na mfumo huo unaoitwa GPX yaani
Global Players Exchange ambao malengo yake ni kurahisisha kufanya
usajili kwa mchezaji.
FIFA imeiandikia barua Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), likitaja klabu tisa za VPL na TFDL
kujisajili kabla ya Jumatatu wiki ijayo kwani itasaidia kupata taarifa
kamili za mchezaji ambayo timu itahitaji kumsajili. Lengo ni kurahisisha
mawasiliano ya usajili kwa mfumo wa Mtandao (TMS-Transfer Matching
System).
FIFA imeleta tu orodha ya timu
ambazo hazijajiunga, lakini TFF ikichambua majina hayo inaona kuwa
majina ya klabu za VPL ni pamoja na African Lyon na Young Africans za
Dar es Salaam, Mtibwa Sugar ya Morogoro, Ruvu Shooting na JKT Ruvu za
Pwani, Mbeya City ya Mbeya, Ndanda ya Mtwara, Kagera Sugar ya Kagera na
Mbao FC ya Mwanza.
Kwa upande wa Ligi Daraja la
Kwanza ya StarTimes zimo African Sports na Coastal Union za Tanga, Marsh
Athletic ya Mwanza, Friends Rangers ya Dar es Salaam, JKT Oljoro ya
Arusha na Polisi Morogoro ya Morogoro.
Timu hizo hazina budi kujiunga na
GPX hadi kufikia Jumatatu ya Septemba 5, mwaka huu. GPX ni kama mtandao
wa kijamii unaoweza kulinganishwa na ‘WhatsApp’ unaofanya kuwa na
mawasiliano ya karibu na FIFA imeagiza kuwa ni lazima mameneja wa TMS wa
kila klabu na mashirikisho ya ya mpira wa miguu kujiunga na mtandao huo
ambao si tu kwamba utafanya kazi katika nchi husika, bali pia
unaunganisha ulimwengu wote.
Kwa mameneja wa usajili wa timu za
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza ya
StarTimes (SFDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) watakaokuwa tayari basi
hawana budi kuwasiliana na Meneja Usajili wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) ili kupata maelezo ya kina ya namna ya kujiunga na mtandao wa
GPX.
0 maoni:
Chapisha Maoni