Waziri Mkuu, Kassim Majliwa
akizungumza na Wafanyabishara na Mabalozi wa Nchi Mbalimbali hapa nchini
kuwaomba wachangie katika kujenga na kukarabati miundombinu
iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.Alikutana nao Ikulu
jijini Dar es salaam Septemba 13, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amepokea michango wa zaidi ya sh. bilioni 1.4 kutoka kwa mabalozi wa
nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara wa Kitanzania
kwa ajili ya kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi
lililotokea Mkoani Kagera.
Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi,
10 Septemba, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 hadi leo na wengine
253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada
ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata nyufa yakiwemo
majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.
Akizungumza katika hafla ya
uchangishaji fedha kwa ajili ya kusaidia wahanga hao leo (Jumanne, 13
Septemba, 2016) Waziri Mkuu amewashukuru kwa michango yao ya fedha na
vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko 2,800 ya saruji. Amesema tetemeko hilo
ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.
Amesema tetemeko hilo
limesababisha Serikali kuzifunga shule zake mbili za sekondari za
Nyakato na Ihungo kati ya nne zilizoathirika vibaya na tetemeko hilo.
“Serikali itajitahidi kuhakikisha
inarejesha miundombini iliyoharibiwa na tetemeko hilo katika kipindi
kifupi ili wanafunzi na wananchi wengine waweze kuendelea na shughuli
zao za kawaida,” amesema.
Waziri Mkuu amesema katika
kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka tayari Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,
Jenista Muhagama yuko mkoani Kagera akiongoza kitengo cha maafa kufanya
thamnili kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.
Mawaziri wengine walioko mkoani
Kagera wakiendelea kufanya tathmini hiyo ni pamoja na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.
Amesema Kamati ya Maafa ya Ofisi
ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya mkoa wa Kagera
imefungua akaunti maalumu katika benki ya CRDB kwa ajili ya kupokea
michango kutoka kwa watu mbalimbali. Namba za akaunti hiyo ya Kamati ya
Maafa ya Kagera ni CRDB 0152225617300.
Pia Waziri Mkuu amewapongeza na
kuwashukuru waheshimiwa Wabunge kwa kuamua kutoa posho zao za kikao cha
leo kwa ajili ya kuchangia wahanga wa tetemeko hilo na kuwaomba wananchi
wengine kujitokeza na kutoa michango yao.
Wakati huo huo viongozi wa
makampuni ya mafuta ya GBP, Oil Com na Moil wameahidi kujenga shule
mbili za Nyakato na Ihungo ambazo sehemu kubwa ya miundombinu yake
imeharibika vibaya. Shule hizo zitajengwa katika kipindi cha siku 30.
Hafla hiyo iliyoongozwa na Waziri
Mkuu ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage,
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk.
Suzan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi, Dk. Aziz Mlima.
0 maoni:
Chapisha Maoni