Posted by Esta Malibiche on Sept.13.2016 in News
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
………………………………………………..
Serikali imeanza kupanga walimu
wa sayansi moja kwa moja katika shule badala ya Halmashauri kama
ilivyokuwa awali ili kuleta uwiano sawa wa walimu katika shule
mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Suleman Jaffo alipokuwa akijibu
swali la Mbunge wa Muleba Prof. Anna Tibaijuka lililohusu mkakati wa
Serikali katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa walimu.
Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa
Serikali imeandaa mkakati wa kuwaajiri wahitimu wa shahada za sayansi
ambazo siyo za ualimu baada ya kuwapa mafunzo ya muda mfupi kuhusu mbinu
za ufundishaji na maadili ya ualimu ili kukabiliana na changamoto ya
walimu wa sayansi nchini.
Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa
tayari kibali kimeombwa katika Ofisi ya Rais Utumishi kwa ajili ya
utekelezaji huo, ambapo Serikali imepanga kuajiri walimu wastaafu wenye
uwezo wa kufundisha waliokuwa wanafundisha masomo ya sayansi kwa mkataba
ili kupunguza pengo lililopo.
Aidha, Naibu Waziri Jaffo
amebainisha kuwa Serikali inafanya tathimini ya mahitaji ya walimu wa
masomo ya sanaa kwa kila Halmashauri ili kubaini maeneo yenye ziada na
yenye upungufu ili kusawazisha.
“Mpango wa Serikali uliopo ni
kuwahamasisha walimu wa ziada wa masomo ya sanaa kwenda kufundisha
katika shule za msingi ndani ya Halmashauri husika, ambapo kabla ya
kuanza utekelezaji wa mabadiliko haya Serikali itatoa waraka maalumu
kwenda katika Halmashauri zote nchini” amefafanua Naibu Waziri huyo.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa
mafunzo ya walimu Mhe. Jaffo amesema kuwa Halmashauri moja haiwezi kuwa
na mfumo wa peke yake wa kuandaa walimu hali ambayo iltakuwa ni vigumu
kuthibiti ubora wa mafunzo hayo kwa walimu.
Hata hivyo amesema kuwa Serikali
itaendelea kuongeza udahili wa walimu wa sayansi katika vyuo vya ualimu
kadri watakavyojitokeza ili kukidhi mahitaji yaliyopo
0 maoni:
Chapisha Maoni