Posted by Esta Malibiche on Sept8.2016 in News
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo macho, haijalala na haijashindwa
kuongoza nchi bali imejipanga kuliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.
“Serikali haijashindwa kuongoza
nchi. Nataka niwahakikishie waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwamba
tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa na kazi hiyo imeanza kwa
marekebisho makubwa kwa maeneo ambayo tunadhani yatafanya Taifa hili
liweze kupata mafanikio makubwa,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Septemba 8, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa
na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Bw. Freeman
Mbowe, ambaye alitaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kunusuru
mdororo wa uchumi uliopo nchini.
Bw. Mbowe alidai kwamba hali ya
uchumi imeshuka na kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
uagizaji wa bidhaa kutoka nje umepungua, uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na
sekta ya ujenzi imesimama hali inayoashiria kudorora kwa uchumi.
Kuhusu suala la kupungua kwa
mizigo katika bandari na vituo vya forodha, Waziri Mkuu amesema
usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bahari umeshuka duniani kote kwa
sababu ya kushuka kwa hali ya uchumi kutokana na kuporomoka kwa bei ya
mafuta na gesi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema
tayari wafanyabiashara wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC) wameihakikishia Serikali kwamba mizigo yao yote itakuwa inapitia
Bandari ya Dar es Salaam hasa kwa mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya
standard gauge inayoanzia Dar es Salaam-Tabora – Isaka.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema
Serikali itahakikisha inaendelea kuimarisha amani na ulinzi kwenye
maeneo yote nchini na kwamba vyombo vya dola viko macho. “Watu wote
wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji watakamatwa popote
walipo na kuchukuliwa hatua za kisheria,; amesema.
Amesema hatua hiyo inatokana na
matukio ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni ambapo raia wasiokuwa na
hatia na askari waliuawa katika maeneo ya Vikindu mkoani Pwani, Tanga na
Mwanza. Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa
Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani
Katika swali lake, Bw. Ngonyani
alitaka kujua ya Serikali kuhusu kukomesha mauaji hayo, yanayotokea kwa
watu wasio na hatia pamoja na askari, ambapo Waziri Mkuu, alitumia
nafasi hiyo kutoa pole kwa wananchi na familia, ambazo ndugu zao
walipoteza maisha katika mauaji hayo.
Pia ametoa wito kwa Watanzania
wote kuhakikisha wanawafichua watu ambao wanawatilia shaka na kutoa
taarifa kwa vyombo vya dola ili waweze kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO, SEPTEMBA 8, 2016
0 maoni:
Chapisha Maoni