Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Mwenyekiti wa Chama cha UDP John
Cheyo amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais
aliyesubiriwa kwa muda mrefu tangu kuanza kwa Uhuru.
Cheyo ameyasema hayo jana alipokuwa akielezea juu ya utendaji wa Rais Magufuli tangu ameingia madarakani Novemba, 2015.
“Utendaji wa Rais Magufuli
umewashtusha watu wengi kwani hawakutegemea kwa muda mfupi aliokuwa
madarakani kama angeweza kuchukua hatua kubwa kama vile kupambana na
mafisadi, jambo ambalo limekuwa likiongelewa na viongozi waliopita
lakini kulikuwa hakuna matunda ya moja kwa moja,” alifafanua Cheyo.
Ameendelea kwa kusema kuwa Rais
Magufuli amekuwa na adhima ya kupambana na Mafisadi na kutatua kero za
Taifa tangu akiwa kwenye kampeni huku akisimamia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.
Vile vile Cheyo amesema kuwa kero
ambazo amekuwa akizitatua Rais Magufuli zikiwemo ufisadi, uchumi
tegemezi, mapato madogo na ukosefu wa vifaa mahospitalini ni kero ambazo
zimekuwa zikipigiwa kelele na kambi ya upinzani kwa muda mrefu.
Hivyo kuingia kwa Rais Magufuli
madarakani kumeleta utatuzi mkubwa kwa kero hizo ambazo zimekosa utatuzi
kwa muda mrefu kutokana na viongozi waliopita kutozichukulia uzito
mfano Rais Magufuli alivyoweza kutatua tatizo la vitanda hospitali ya
Taifa ya Muhimbili kwa kipindi kifupi ambapo hivi sasa hakuna mgonjwa
anayelala nchini katika hospitali hiyo.
Akielezea suala la ufisadi nchini,
Cheyo amesema kuwa ufisadi ni ugonjwa wa muda mrefu ambao umepoteza
fedha nyingi za nchi kutokana na mikataba mibovu iliyokuwa ikisainiwa na
viongozi wa juu.
Aidha amempongeza Mhe. Rais kwa
kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kuona tatizo hilo lishughulikiwe
kisheria na kwa njia maalum ili kukomesha ufisadi nchini.
Cheyo amewataka watanzania kugeuza
mawazo yao na kuchukia rushwa kwa kukataa kupokea na kutoa rushwa kwani
rushwa ni adui wa haki na inarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
0 maoni:
Chapisha Maoni