Posted by Esta Malibiche on Sept4.2016 in SIASA
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
kimeipongeza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanzia Dkt.
John Pombe Magufuli aliyotoa katika ziara zake Zanzibar, iliyosisitiza
dhamira ya serikali kuharakisha maendeleo kwa wananchi bila ya kujali
tofauti za kisiasa.
CCM imesema inaunga mkono na
kupongeza kwa dhati hotuba hizo zilizotolewa Unguja na Pemba
ziliyosisitiza dhamira ya serikali zote mbili ya jamhuri ya muungano wa
Tanzania na Zanzibar kuwaletea wananchi maendeleo bila ya kujali itikadi
za kisiasa.
Akizungumza Katibu wa Kamati
Maalum ya NEC Zanzibar wa Idara ya ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari
Jabu alisema viongozi na wananchi kwa ujumla wanatakiwa kushirikiana
katika ujenzi wa maendeleo ya nchi ili zanzibar iweze kufikia hadhi ya
kuwa nchi yenye uchumi mkubwa katika nchi za Afrika.
Waride alieleza kwamba ziara hiyo
imetoa muongozo imara wa kuwakumbusha watendaji na viongozi nchini juu
ya dhamana na mambo ya msingi wanayotakiwa kuyatekeleza kwa wananchi.
“CCM tunaunga mkono kwa nguvu zote
hotuba ya Rais wetu Dkt. John Magufuli kwani imezungumzia na kugusia
mambo ya msingi yanayogusa maisha ya wananchi hasa wa kipato cha chini
na kutoa muongozo wa namna gani serikali zetu zinaendelea na mikakati
imara ya kuimarisha uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Pia tunatakiwa kuendelea kuwa
wamoja na wazalendo bila ya kujali tofauti zetu za kidini, kisiasa na
kikabila kwa kulinda amani na utulivu wa nchi zetu kwani ndio siri ya
mafanikio ya nchi zetu.”, Alisisitiza Waride.
Katibu huyo , alisema Dkt.
Magufuli ameonyesha nia ya dhati ya kuendelea kutafuta fursa mbali mbali
za miradi ya maendeleo itakayoweza kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.
Alisema miongozo mwa mambo ya
msingi yaliyosisitizwa na Dkt. Magufuli pia yanaungwa mkono na CCM
Zanzibar ni dhamira ya kuhakikisha Zanzibar inakuwa ni nchi ya Viwanda
vya kusindika samaki wanaotokana na Uvuvi wa Kisasa wa Bahari kuu
vitakavyotoa fursa za ajira kwa vijana na wananchi.
Waride, alipongeza juhudi
zinazofanywa na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua milango
ya wawekezaji wakubwa kuwekeza Zanzibar huku wakitafuta wahisani kutoa
mamilioni ya fedha za kuendesha miradi ya kijamii ukiwemo mradi wa maji
safi Unguja uliotolewa fedha za mkopo na Serikali ya India.
Alisema kwa ushirikiano wa Rais
Dkt. Magufuli na Dkt. Shein, CCM inaamini kwamba Tanzania bara na
Zanzibar kwa ujumla zitakuwa nchi za kupigiwa mfano duniani katika
nyanja mbali mbali za kimaendeleo, kisiasa na kijamii.
Alifafanua kwamba CCM Zanzibar,
inaungana na Dkt. Magufuli kupinga siasa za misimamo mikali na utengano
zinazofanywa na baadhi ya vyama vya kisiasa Zanzibar kuwa haziwezi
kuleta maendeleo ya nchi badala yake zitajenga migogoro isiyokuwa ya
lazima.
Alisema CCM inasifu msimamo wa
Dkt. Magufuli wa kulinda Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964
huku akiahidi kuendelea kulinda amani na Utulivu wa nchi kwa gharama
yoyote.
Pamoja na hayo Waride aliahidi
kuwa CCM itaendelea kuwa balozi mzuri wa kuwasihi wafuasi wa chama hicho
na wananchi kwa ujumla kufanya siasa za maendeleo zitakazoweza kwenda
sambamba na malengo ya serikali.
Aidha Waride alipongeza juhudi za
Rais wa Zanzibar, Dkt. Shein za kuongoza nchi kwa ufanisi mkubwa licha
ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kisiasa nchini.
Alielezea kuridhishwa kwake na
kauli ya Dkt. Shein ya kuwataka wapinzani kusahau Serikali ya Mpito
kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi huku akisisitiza hakuna sababu ya
kuwa na aina ya serikali hiyo kwa sababu uchaguzi umefanyika kwa njia
ya huru na haki.
Katika Mkutano huo, Dk Shein
alisema kazi kubwa inayofanywa kwa sasa ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya Mwaka 2015, huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa
katika hatua ya mwisho ya kuanza kazi za kuchimba mafuta na ges ili
kutoa hatua pana ya ajira kwa wananchi.
Alisema muswada wa mafuta na gesi
tayari umewasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na kusomwa kwa mara ya
kwanza ambapo katika kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi
kitakachofanyika Septemba 26 utasomwa kwa mara ya pili na kusubiri saini
yake.
Ziara hiyo ya Dkt. Magufuli ya
kuwashukru wananchi wa Zanzibar kwa kumchagua kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika uchaguzi Mkuu uliopita, imefanyika katika
maeneo mbali mbali Pemba na Unguja.
0 maoni:
Chapisha Maoni