Posted by Esta Malibiche on Oct6.2016 in BIASHA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Watumishi wa Mamalaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)
kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Oktoba 6, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Baadhi ya Watumishi wa Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Mkuu CDA wakimsikilizwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Oktoba
6, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya Watumishi wa Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Mkuu CDA wakimsikilizwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Oktoba
6, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………….
*Kiwanja chauzwa kwa sh. milioni 240 lakini zilizoingia CDA ni milioni 6 tu
*Ahimiza kasi ya upimaji viwanja, asema waliolipa nusu wasinyang’anywe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Bw.
Uledi Mussa afuatilie malipo ya kiwanja kilichouzwa na CDA kwa sh.
milioni 240 lakini fedha iliyoingia ofisini ni sh. milioni 6 tu.
“Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri
Mkuu, ninataka ufuatilie mauzo ya kiwanja namba 26 block AA eneo la
Kikuyu East ambacho kimeuzwa kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia
CDA ni sh. milioni 6 tu. Nataka kujua nani ameingiza milioni 6 na nani
kachukua hizo sh. milioni 234,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
mchana (Alhamisi, Oktoba 6, 2016) wakati akizungumza na watumishi na
viongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwenye
ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Bila kutoa ufafanuzi zaidi,
Waziri Mkuu amesema eneo hilo lilipaswa kuwa na kituo cha mafuta na
akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo.
Pia amemwagiza Katibu Mkuu huyo
afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo la CDA ambalo wamepangishwa
taasisi ya Tunakopesha Limited kwa madai kuwa mhusika alipewa bure na
sasa anataka kulipangisha tena ili apate cha juu.
Waziri Mkuu amewaonya watumishi
hao pamoja na viongozi wao waache tabia ya kushirikiana na madalali
kuuza viwanja na akawataka wachape kazi wakijielekeza na kasi ya
Serikali ya kuhamia Dodoma.
“Tabia ya watumishi kushirikiana
na madalali kuuza ardhi sasa basi. Hata hivyo, nimefarijika kukuta
mmeanza kuweka mfumo wa kielektoniki katika baadhi ya huduma. Ni lazima
mauzo ya viwanja sasa hivi yafanyike kwa njia ya kieletroniki, madalali
hawana nafasi,” amesisitiza.
Ameutaka uongozi wa CDA uongeze
kasi ya upimaji viwanja kwa sababu mahitaji ni makubwa lakini akaonya
kuwa wakati zoezi hilo likifanyika, wananchi walionunua viwanja na bado
hawajamalizia kuvilipia, wasinyang’anywe kwa kigezo cha kutaka kuwauzia
wengine.
“Mimi nataka idadi ya viwanja
vilivyopimwa iongezeke. Lakini pia msitumie fursa hii kuwanyang’anya
watu wenye umiliki halali eti kwa sababu Serikali inataka idadi ya
viwanja vilivyopimwa iongezeke,” amesema.
“Kama mtu amepewa offer
au hati yake asinyang’anywe hata kama amelipia nusu asinyang’anywe.
Ahimizwe kumalizia hilo deni na ninyi kazi yenu ni kupima viwanja
vingine,” amesisitiza.
“Natambua mnayo benki ya viwanja,
lakini inabidi muongeze idadi ya viwanja vingi zaidi. Tumeita
wawekezaji waje kujenga nyumba za kuishi watumishi, mahoteli na viwanda
na maeneo yote haya inabidi yatengwe rasmi,” amesema.
Amesema jumla ya viwanja 70,000
vimepimwa tangu CDA ianzishwe mwaka 1973. Amesema kama wataendelea na
kasi hiyo wakati mahitaji yameongezeka, itawachukua zaidi ya miaka 40
kukamilisha mahitaji ya viwanja 100,000 ambavyo vinatarajiwa kuanza
kupimwa hivi karibuni.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya
Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Eng. Paskasi Muragili amesema
usanifu wa upimaji viwanja 20,000 umekamilika na kwamba wana lengo la
kupima viwanja vingine 100,000 ifikapo Juni 2017.
Waziri Mkuu alitembelea Ofisi ya
CDA na kukagua mfumo wa utunzaji mafaili wa zamani pamoja na uhamishaji
wa taarifa za wenye viwanja kwenye mfumo wa kompyuta. Pia alikagua
mifumo ya uuzaji viwanja kwa njia ya mtandao ambayo hata hivyo bado
haijakamilika.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amepokea mchango wa zaidi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Wilaya
wa Kongwa, Bw. Deogratius Ndejembi zikiwa ni kwa ajili ya wakazi wa mkoa
wa Kagera walioathirika kwa tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10,
mwaka huu.
Pia Waziri Mkuu amepokea mchango
mwingine wa zaidi ya sh. milioni tano kutoka kwa makundi mbalimbali ya
wafanyabiasha wa Manispaa ya Dodoma wakiwemo wamiliki wa hoteli, nyumba
za kulala wageni, waendesha bodaboda na madereva wa daladala.
Akipokea msaada huo, Waziri Mkuu
amewashukuru wafanyabiashara hao na kuwahakikishia kwamba fedha hizo
zitapelekwa mkoani Kagera na kuwafikia walengwa kama ilivyokusudiwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni