Naibu Waziri Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Walemavu Dkt. Abdallah
Possi akiongea na wageni waalikwa hawapo pichani wakati wa uzinduzi wa
taarifa mpya ya utafiti inayobainisha hali halisi ya ulemevu na uzee
nchini jijini Dar es salaam.
……………………………………………………..
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO
Watafiti wa masuala mbalimbali ya
kijamii nchini wametakiwa kuhakikisha wanafanya tafiti ambazo
zitawasaidia watu wenye ulemavu kupata vifaa saidizi ili waweze kumudu
kuendesha maisha yao ya kila siku.
Hayo yamebainishwa na Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye
Walemavu Dkt. Possi Abdallah alipokuwa akizindua taarifa mpya ya utafiti
inayobainisha hali halisi ya ulemevu na uzee nchini jijini Dar es
salaam.
“Serikali inafarijika inapoona
watu wanafanya utafiti ili kuwasaidia watu wenye ulemavu waweze kupata
vifaa saidizi na ni kitu gani kifanyike ili NGOs ziweze kujikwamua
kiuchumi na kuwasaidia wenye mahitaji” alisema Dkt. Possi.
Kuhusu suala la unyanyapaa kwa
watu wenye ulemavu, Dkt. Possi amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu hapo
tayari kuona wananchi wananyanyapaliwa huku akisisitiza kuwa watu wote
ni sawa na ofisi hiyo ina “zero tolerance” kwa watu wanaowanyayapaa
mlemavu.
Katika masuala ya kisheria kwa
watu wenye ulemavu, Dkt. Possi amesema kuwa inapotokea mlemavu au mzee
amefanyiwa kosa taarifa itolewe mara moja ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi ya waliofanya makosa hayo na haki iweze kutendeka.
Naibu Waziri Dkt. Possi pia
amezitaka Asasi zinazoshughulika na watu walemavu wafanye kazi kwa
pamoja ili kuwasaidia walengwa ambao ni walemavu, watoto na wazee na
kuwataka kutumia fursa waliyonayo ya kupata msaada kisheria bure kutoka
kwenye taasisi za sheria ikiwemo Chama cha Mawakili (Tanganyika Law
Society), TAMWA pamoja na taasisi nyingine za kisheria wakati masuala
ya jianai amewataka wayapeleke kwenye polisi kwa hatua zaidi za kisheria
huku akisisitiza kumshirikisha inapobidi kufanya hivyo.
Akitoa maelezo ya utafiti huo
wakati wa uzinduzi, mtafiti kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) Bakar
Fakih amesema kuwa utafiti huo umewashirikisha watafiti rika mbalimbali
wakiwemo wazee na watu wenye ulemavu na kubainisha kuwa bado kuna imani
potofu kwenye jamii juu ya wazee na watu wenye ulemavu.
Utafiti huo unaoongozwa na
kaulimbiu “Ulemavu na uzee sio laana” umebainisha kuwa watu wenye
ulemavu na wazee nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
kupata elimu, huduma za afya, unayanyasaji wa kingono na kuvunjika kwa
ndoa, kutokujaliwa na familia pamoja na kutengwa kwa watu wenye ualbino
kutokana na mila potofu.
Kwa upande wake mtafiti rika
Blandina Isaya amesema kuwa walemavu waachwe wafanye maamuzi yanayohusu
maisha yao ikiwemo masuala ya ndoa wawe huru kuchagua wenza wao badala
ya kuchaguliwa na familia zao kwa kuwa wanahaki kama watu wengine wasio
na ulemavu.
Katika kuhakikisha familia
zinakuwa imara kiuchumi, Blandina amesema kuwa familia zenye watu wenye
ulemavu na wazee wapewe elimu ya ujasiriamali ili waweze kuwa na uwezo
wa kuendesha maisha yao kwa kulea familia ipasavyo na kuomba Seriklai za
mtaa ziwe na takwimu za wazee na watu wenye ulemavu.
0 maoni:
Chapisha Maoni