Posted by Esta Malibiche on Oct13.2016 in NEWS
Na Beatrice Lymo- MAELEZO
“Uhai wa wanyamapori ni jambo
linalotuhusu sisi sote katika Afrika, viumbe hai wa porini wakiwa katika
mapori waishimo sio muhimu tu kwa ajili ya kuajabiwa na kuvutia lakini
pia ni sehemu ya maliasili yetu na mustakabali wa maisha yetu baadaye”
Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere alisema hayo wakati akitoa tamko la Arusha kuhusu Uhifadhi wa
wanyamapori kipindi Tanganyika inapata Uhuru mwaka 1961.
Alisema kwa kukubali dhamana ya
wanyamapori, watanzania watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wajukuu
na watoto wa kitanzania wanaweza kufurahia urithi mkubwa wa thamani hiyo
adimu ya wanyamapori.
Juhudi za uhifadhi na kulinda
rasilimali, malikale na kuendeleza shughuli za ufugaji nyuki pamoja na
kukuza Sekta ya Utalii ikiwa ni jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii
zilikuwepo hata kabla ya ukoloni ambapo jamii nchini zilitenga mapori
kwa ajili ya kuabudia na kutambika.
Kuingia kwa wakoloni nchini
kuliambatana na kutunga Sheria za uhifadhi wa rasilimali za maliasili na
malikale ambapo ni Sheria ya kuhifadhi Majengo ya kihistoria ya mwaka
1937, Sheria ya Makumbusho ya mwaka 1941, Sheria ya Usimamizi wa Misitu
ya mwaka 1957, Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ya mwaka 1959, Sheria ya
Hifadhi za Taifa ya mwaka 1959 na Sheria ya kuhifadhi wanyama ya mwaka
1959.
Chini ya uongozi wa Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere, kuanzia mwaka 1961 Wizara ya Maliasili na
Utalii imekuwa na Sera na Sheria tofauti kulingana na mabadiliko
yaliyokuwa yakitokea duniani katika nyanja za kiuchumi, kiteknolojia,
kiasiasa na kijamii.
Juhudi za Baba wa Taifa katika
kuhakikisha Sekta ya utalii ambapo ilikuwa na idara moja mwaka 1961
kuanza kuwa na Sera ya uhifadhi wa maliasili, malikale na kuendeleza
utalii nchini zinaonekana.
Mabadiliko na matukio makuu ya
Wizara ya Maliasili na Utalii mara baada ya uhuru mwaka 1961 yalipelekea
jitihada za makusudi za kuwezesha wazawa kielimu ili kuweza kuchukua
nafasi za utendaji na uongozi ambazo awali zilishikiliwa na wageni.
Aidha, mwaka 1967 kufuatiwa
kupitishwa Azimio la Arusha chini ya uongozi wa Baba wa Taifa mali
binafsi zilitaifishwa na kuundwa kwa mashirika na taasisi za umma ambapo
Wizara iliunda mashirika ya umma ikiwemo Shirika la Wanyamapori,
Shirika la Viwanda vya mbao, Shirika la Utalii Tanzania, Shirika la
kuhudumia wasafiri na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la
kukuza na kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Katika mabadiliko hayo ndani ya
Wizara, juhudi za Mwalimu Nyerere zilipelekea Serikali kujitoa katika
kuendesha shughuli za kibiashara na kujikita katika kusimamia Sera na
uwezeshaji.
Kadhalika katika suala la ulinzi
wa rasilimali za maliasili, Serikali ilirithi mfumo wa ukoloni ambapo
Serikali ilikuwa ndiye mlinzi na mwendelezaji mkuu wa rasilimali za
maliasili, malikale na utalii ambapo mabadiliko ya kisera na mwelekeo wa
uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali ulifanyika miaka ya 1991 kwa
kuhimiza ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi na uendelezaji wa
rasilimali za maliasili, malikale na utalii.
Ushirikishwaji jamii katika
shughuli za maliasili na utalii ulichangia katika Wizara kuanzisha
vitengo mbalimbali ikiwemo kitengo cha Ugani katika idara na taasisi
zake ikiwa na lengo la kuimarisha na kukuza sekta ya utalii nchini.
Vilevile, katika suala la ajira
na jinsia katika wizara, wakati nchi inapata uhuru sekta za maliasili
hususani wanyamapori, misitu, malikale na nyuki zilikuwa maalumu kwa
wanaume ambapo juhudi za Mwalimu Nyerere ziliwezesha kupatikana kwa
ajira ikihusisha jinsia zote mbili, ambapo sekta ya utalii ikaajiri
mwanamke kwa mara ya kwanza mwaka 1970.
Katika sekta ya nyuki wanawake
wawili waliokuwa na astashahada ya ufugaji wa nyuki waliajiriwa mwaka
1975, sekta ndogo ya misitu iliajiri mwanamke wa kwanza mwenye shahada
mwaka 1976, katika sekta ndogo ya wanyamapori mwanamke aliajiriwa mwaka
1967 na katika sekta ya mambo ya kale mwanamke aliajiriwa mwaka 1978 kwa
ngazi ya cheti na 1981 kwa ngazi ya shahada.
Kama Mwalimu Nyerere, Rais John
Pombe Magufuli naye ameonyesha kukerwa na vitendo vya ujangili na
biashara haramu ya kuuza meno ya tembo. Katika hotuba zake Mhe. Rais
Magufuli amekuwa akisisitiza utunzaji wa maliasili kwa ajili ya maendelo
ya Taifa.
Pia katika kuongeza tija na
kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa zilizofanyiwa utafiti, wizara
ilianzisha vyuo vya ulinzi, uhifadhi na uendelezaji wa maliasili,
malikale na utalii ambapo chuo cha viwanda vya misitu kilianzishwa mwaka
1975, chuo cha ufugaji nyuki Tabora mwaka 1978 pamoja na vyuo vya elimu
ya wafanyakazi Rongai na Sao Hill vilivyoanzishwa mwaka 1979 kwa lengo
la kutoa elimu ya awali ya uoteshaji miche na kuhudumia misitu.
Katika kukuza na kuimarisha sekta
ya utalii nchini Mwalimu Nyerere aliweza kutekeleza majukumu ya wizara
kulingana na mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea nchini na duniani
katika nyanja ya kiuchumi, kisiasa kiteknolojia na kijamii.
Juhudi hilo zilipelekea wizara
kuongeza vituo vya malikale na kutangaza maeneo tofauti kama urithi wa
Taifa, mashamba ya miti yaliongezeka, misitu ya asili pamoja na hifadhi
za Taifa kuongezeka.
Mbali na hayo juhudi za Mwalimu
katika kukuza na kuimarisha sekta ya utalii mara baada ya uhuru
zilichangia katika ongezeko la mikusanyo ya malikale ambapo wakati wa
uhuru wizara ilihifadhi jumla ya mikusanyo 10,151 ya fani za Akiolojia,
mila, historia, bayolojia na nyaraka mbalimbali.
Aidha baada ya uhuru kutokana na
tafiti zilizofanywa na watafiti wazawa na wageni kutoka nje ya nchi hadi
juni, 2011 wizara imefanikiwa kuhifadhi nchini urithi wa malikale
unaohamasisha wenyeji jumla ya mikusanyo 337,361.
Katika suala la ongezeko la idadi
ya watalii wanaongia nchini ndani ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere
idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 9,847 mwaka 1960 hadi
watalii 103,361 mwaka 1986.
Mbali na hayo katika kuendeleza
jitihada za kukuza na kuimarisha sekta ya utalii nchini, Rais Mstaafu wa
awamu ya tatu Benjamin Mkapa, kwenye Sherehe ya kilele cha Mbio za
Mwenge wa Uhuru, wiki ya Vijana na Kumbukumbu ya Baba Wa Taifa, Mwalimu
Julius K. Nyerere, Singida mwaka 2005 alisema kuwa sekta ya utalii ni
muhimu katika ukuzaji wa uchumi wetu hivyo ni budi kuitunza na
kuithamini.
“Ukweli unaojionyesha ni kwamba
kama tukijikita katika sekta hii tunaweza kuongeza kasi ya ukuaji wa
uchumi katika nchi yetu, nategemea kwamba sekta hii inaweza ikatuongezea
mchango wake katika pato la Taifa hivyo tutumie rasilimali zilizopo
kuwavutia watalii na wawekezaji wengine kuingia katika sekta hii”,
aliongeza Rais Mkapa.
Alibainisha kuwa hifadhi ya
mazingira ni eneo ambalo linahitaji nguvu za pamoja na za haraka katika
kuepusha athari zinazoweza kutokea kama hatujali na kutilia maanani
hivyo jamii inahitaji kuhifadhi misitu, vyanzo vya maji na kupanda miti
kwa wingi ili kuzuia nchi kuwa jangwa.
Kwa upande wake Rais Mstaafu wa
Awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ali Hassan Mwinyi
hivi karibuni alitoa wito kwa watanzania kuongeza juhudi katika
kusaidiana na Serikali kupiga vita ujangili hapa nchini kwa lengo la
kuimarisha sekta hiyo.
Rais mstaafu huyo, alisema
kumekuwa na tatizo la mauaji ya wanyamapori hapa nchini ambayo ni dhambi
na ni kinyume na kusudio la Mungu kwa kuwa wanyama hao wana haki ya
kuishi kama viumbe wengine.
“Kumekuwa na matukio mengi ya
uuaji wa wanyamapori ikiwemo tembo na faru na hivyo kupunguza rasilimali
ya taifa kwa vizazi vijavyo na pia kitendo hicho ni kinyume na kusudio
la Mungu hivyo ni vizuri kuwatunza, kuwapenda, kuwaendeleza na kuwalinda
wanyama hao kwani ni moja ya vivutio vinavyochangia pato la Taifa”
aliongeza Rais Mstaafu Mwinyi.
Nae Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein katika sherehe
za miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar aliwataka Wananchi kutumia vivutio
vya utalii vilivyopo ili kuweza kukuza utalii wa ndani kwani kwa pamoja
taifa litaendeleza juhudi za kukuza sekta ya utalii kwa kauli mbiu ya
“Utalii kwa wote” ili iendelee kuwa na mchango mkubwa katika soko la
ajira, kuingiza fedha za kigeni na katika kukuza Pato la Taifa kwa
jumla.
Sambamba na hilo Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema asilimia 80ya
mapato ya fedha za kigeni zinazoingia nchini kupitia Sekta ya Utalii
inaweza kubakia kuwa ndoto kama suala la amani na utulivu
halitazingatiwa na kupewa nafasi yake chini ya usimamizi wa Jamii kwa
mashirikiano na Serikali Kuu.
Alisema hakutakuwa na mgeni wala
mtalii atakayekuwa na shauku ya kutaka kuingia nchini sambamba na
kufifia biashara ya Utalii endapo amani na utulivu uliopo utachezewa na
hatimae kutoweka kabisa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa kumekuwa na changamoto
zilizohusu masuala ya Maliasili na Utalii zilizojitokeza wakati wa
kampeni ikiwemo ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki, Migogoro
ya mipaka kati ya vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato hivyo kuahidi
kuzifuatilia changamoto hizo ili kuweza kukuza na kuimarisha sekta ya
utalii nchini.
Mbali na hayo wakati akitoa
hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la Jamhuri Rais Magufuli aliwataka
mabalozi wanaowakilisha Tanzania nchi za nje kutumia fursa walizo nazo
katika kutangaza utalii wa nchi ili kuweza kuongeza pato la Taifa.
Wizara ya Maliasili na Utalii
inaendelea kutekeleza majukumu yake licha ya mabadiliko na changamoto
mbalimbali na inatarajiwa kuwa rasilimali za maliasili, malikale na
utalii zitaendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa juhudi za kukuza uchumi
wa Taifa.
Hakika Mwalimu Nyerere mchango
wake kwa sekta ya utalii haiwezi kusahaulika, itakumbukwa vizazi hadi
vizazi. Utalii ukitiliwa mkazo na kuboresha miundombinu ya kuwawezesha
watalii kufika na kukaa bila taabu ni dhahiri watalii wataongezeka na
hivyo kukuza Pato la Taifa.
0 maoni:
Chapisha Maoni