Mtaalamu wa macho kutoka China
Dkt. Zhao Wei akimpima macho Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo kwenye
maadhimisho ya siku ya uoni Duniani yaliyofanyika kitaifa kituo cha Afya
cha Magogoni, Mjini Zanzibar.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza
kupima macho kwenye maadhimisho ya siku ya uoni Duniani yaliyofanyika
Kituo cha Afya Magogoni wakiendelea kuangaliwa macho.
Mratibu wa huduma za macho
Zanzibar Dkt. Rajab Mohammed Hilal akisoma risala ya kitego cha matibabu
ya macho kwenye maadhimisho ya siku ya uoni Duniani yaliyofanyika Kituo
cha Afya Magogoni, Mjini Zanzibar.
Mwakilishi wa Shirika la
Sightsaver Tanzania Andrew Kilewela akibadiliishana mawazo na Mratibu wa
Mradi wa Afya ya macho Zanzibar Dkt. Fatma Juma Omar wakati wa
maadhimisho ya siku ya uoni Duniani katika Kituo cha Afya Magogoni.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit
Kombo akizungumza na wananchi na wafanyakazi wa Kituo cha Afya Magogoni
kwenye maadhimisho ya siku ya uoni Duniani yaliyofanyika katika Kituo
hicho.
………………………………………………………………………
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit
Kombo amewataka wananchi kuendelea kuvitumia vituo vya afya vilivyo
karibu nao vinavyotoa huduma za macho katika jamii ili kupambana na
upofu usiowalazima.
Amesema vituo vingi vya Afya hivi
sasa vimewekewa huduma muhimu za uchunguzi wa maradhi mbali mbali,
ikiwemo uchunguzi wa macho, na hakuna haja ya wananchi kukimbilia
Hospitali Kuu ya Mnazimmoja.
Waziri Mahmoud ameeleza hayo
katika maadhimisho ya siku ya uoni Dunini yaliyofanyika Kitaifa kituo
cha Afya Magogoni Wilaya ya Magharibi B.
Amesema madaktari wanapohisi
tatizo ni kubwa na haiwezekani kupata matibabu katika vituo vidogo
wanaamua kumpeleka mgonjwa Hospitali Kuu hivyo hakuna haja ya kuwa na
wasiwasi na viituo hivyo.
Amesema tatizo la uoni limekuwa
kubwa duniani kote na inakisiwa hivi sasa kuna watu wasioona wapatao
milioni 285 na asilimia 37 kati yao hawaoni kabisa.
Kwa upande wa Zanzibar amesema
inakisiwa kuwa na watu 10,000 ambao wanamatatizo ya uoni na asilimia 50
kati ya hao hawaoni kabisa kutokana na sababu mbali mbali.
Waziri wa Afya ameongeza kuwa
wataalamu wa maradhi ya tiba ya macho nchini kwa kushirikiana na Shirika
la Afya ulimwenguni (WHO) pamoja na taasisi mbali mbali duniiani wako
katika mikakati ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya maradhi ya macho.
Hata hivyo amesisitiza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya inajitahidi
kuendeleza huduma za matibabu ya macho katika nyanja zote katika vijiji
mbali mbali Unguja na Pemba kupitia Kitengo chake cha Afya ya msingi ya
matibabu ya macho vijijini.
Amewataka wananchi kufanya juhudi
kuepuka maradhi ambayo yanapelekea matatizo ya macho na kujenga
utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara kwani ni moja ya tiba ya
kujiepusha na maradhi mengi.
Aidha alilishukuru Shirika la
Kimataifa la Sightsaver kwa ushirikiano wake wa karibu na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na misaada ya kitaalamu na dawa wanazosaidia
kitengo cha matibabu ya macho.
Katika risala ya wafanyakazi wa
Kitengo cha matibabu ya macho iliyosomwa na Mratibu wa Kitengo hicho
Dkt. Rajab Mohammed Hilal wamesema wanakabiliwa na udogo wa nafasi ya
kutekeleza katika kitengo hicho.
0 maoni:
Chapisha Maoni