Posted by Esta Malibiche on Oct 28.2016 in SIASA
Ndugu Christopher Ole Sendeka,
Msemaji wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa akizungumza kwenye
mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo tarehe 28/10/2016
katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba
jijini Dar es salaam.
………………………………………………………….
Kwa muda sasa kumekuwepo na
usambazaji wa taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa
wakishirikiana na baadhi ya vyombo vya habari zinazolenga kukejeli,
kudhihaki, kukatisha tamaa, kubeza na kudhoofisha jitihada zinazofanywa
na Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake katika kuleta maendeleo kwa
Watanzania.
Kumekuwepo na makala
zinazoandikwa na magazeti mawili ya nje ambazo hutolewa kila baada ya
miezi miwili na ambazo zinapotosha na kuandika habari zisizo za kweli
kuhusu Tanzania.
Pia, yapo magazeti mawili ya
ndani ambayo yamekuwa yakitoa makala mfululizo kwa kila wiki zinazolenga
kumchafua Mheshimiwa Rais na kuichafua taswira ya nchi yetu.
Tumesikitishwa na waandishi wa
makala hizo walioamua kujivua uzalendo na kushiriki mpango wa kuiharibu
heshima na taswira ya nchi yetu kwa maslahi ya maadui zetu wa nje na
baadhi ya wanasiasa. Tunafuatilia kujua nini kinawasukuma kufanya hivyo
na kwa maslahi ya nani ilhali sote ni Watanzania. Je ni tamaa ya
madaraka tu au mengine? Hakuna anayepinga ukosoaji bali unapaswa uwe
ukosoaji wenye nia njema kwa nchi.
Mtakumbuka hivi karibuni
aliyewahi kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu
ya CHADEMA, Edward Lowassa, alisambaza taarifa kwa vyombo vya habari
aliyoiita ya tathmini ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba
25, 2015.
Katika taarifa yake hiyo, alidai
kuwa alileta msisimko mpya katika siasa za Tanzania, kwamba
ameshirikiana na wenzake kuionyesha nchi yetu maana ya demokrasia na
kukosoa juhudi za serikali na wateule wa Rais.
Demokrasia kimsingi ni dhana
inayohusisha ushiriki na kuheshimu mawazo ya wengi katika kufikia
uamuzi. Ikiwa maana halisi ni hii, tunajiuliza ni ipi demokrasia
aliyoionyesha Lowassa ambayo leo anajisifu kuwa nayo?
Tulishuhudia akiwa
mgombea urais wa chama ambacho hakijui, hakushiriki kukijenga wala kutoa
mchango wowote unaompa hadhi ya kupeperusha bendera huku katiba na
kanuni ya chama hicho ikivunjwa. Kidemokrasia, anayepewa fursa ya
kupeperusha bendera ya chama chochote makini duniani ni kiongozi au
mwanachama aliyethibitika kwa imani na matendo, kuzielewa, kuzitekeleza,
kuzitetea falsafa, itikadi na malengo ya msingi ya chama hicho. Mgombea
ni taswira halisi na alama muhimu inayoakisi dhamira ya chama husika
machoni kwa wananchi
Demokrasia ya kweli
lazima ianzie ndani ya chama, ni demokrasia ipi iliyotoa mamlaka kwa
vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba ridhaa ya
kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea, kuvigharamia na
walivyovitumikia kwa kuamua kumteua mgombea “MTUNGUO” (ambaye
hajapimwa wala hajawahi kuvipigania). Kitendo hicho cha kutowashirikisha
wanachama na kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa
kilidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia.
CHADEMA watuambie njia
iliyotumika kuwapata wabunge wa viti maalumu. Ni demokrasia gani
inayotoa fursa kwa baadhi tu ya viongozi kuteua wabunge ambao
wanakiwakilisha chama chote. Ambapo kila kiongozi aliteua maswahiba zake
na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA walikosa watu wanaowafahamu
na kuamua kuwateua wanawake maswahiba wao ndani ya CCM. Msingi wa
kawaida wa kupata wabunge wa viti maalum ukiacha kura za maoni, kigezo
kingine muhimu ni mchango wa mgombea/mwanachama huyo katika kukijenga na
kukitumikia chama chake. Yaliyotokea kwa CHADEMA kwenye wabunge wake wa
viti maalum ni mapya kwenye ulimwengu wa demokrasia. Inahitaji
wataalamu wa sayansi ya siasa kufanya utafiti wa aina hii mpya ya
demokrasia.
Tulidhani baada ya mwaka mmoja
kupita, wenzetu hawa wangelikuwa wamejifanyia tathmini, kujikosoa,
kujisahihisha na hata kufanya uungwana wa kuwaomba radhi wanachama wao
kwa uvunjifu mkubwa wa misingi ya demokrasia, katiba na kanuni za vyama
vyao.
Tunatoa wito kwa vyama vya siasa
nchini kutochukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko,
yasiwe ni nyimbo za kuburudisha au kutoa matumaini hewa kwa wanachama na
wananchi. Kanuni mojawapo ya demokrasia ndani ya vyama ni lazima
ionekane katika muundo wake na katika utekelezaji wa muundo huo.
Umefika wakati vyama vya siasa
vinapaswa kujifunza kuuza sera ili kujijenga na sio kusubiri matukio kwa
ajili ya kupata huruma ya wananchi. Tunasubiri kushuhudia na kusikia
demokrasia itakavyoendeshwa katika uchaguzi wa ndani wa vyama hivyo
ambapo kuna taarifa mmoja wa vigogo amefanikiwa kupata kiasi cha dola
milioni 15 zitakazomsaidia kupanga safu yake ya uongozi.
Katika kutimiza mpango huo,
tayari yapo mawasiliano ya mara kwa mara ya baadhi ya viongozi wakitoka
Zanzibar na sehemu zingine za nchi kuja Dar es Salaam, na imeonekana
dhahiri mazungumzo yao kutowashirikisha viongozi wenzao waandamizi kwani
yanalenga kufanikisha mpango huo.
Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe
Magufuli, ameendela kufanya juhudi kubwa katika kuijenga nchi kwa
kuimarisha utendaji na nidhamu ya utumishi serikalini, kukusanya mapato
na kusimamia matumizi sahihi ya fedha, kupambana na kuzuia mianya ya
rushwa pamoja na kusimamia haki, usawa na wajibu kwa raia. Mwenzetu
anayaona haya kuwa ni kuufanya utumishi wa umma kaa la moto.
Juhudi hizi na nyinginezo ikiwemo
ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, afya
kwa kununua vitanda vya wazazi, kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi
hadi sekondari na nyinginezo hazipaswi kukatishwa tamaa kwa maslahi ya
wachache, ni vyema kuziunga mkono kwa maslahi ya taifa letu.
Katika kipindi hiki cha mwaka
mmoja wa Rais Dk. Magufuli madarakani, CCM inawaomba wananchi kuendelea
kumuunga mkono katika dhamira yake safi ya kuwaondolea kero, kuboresha
huduma za jamii na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
CHRISTOPHER OLE SENDEKA
MJUMBE WA NEC NA MSEMAJI WA CCM
28/10/2016.
0 maoni:
Chapisha Maoni