Posted by Esta Malibiche on Oct10.1016 in NEWS
Na Ally Daud-MAELEZO
DAWA muhimu za binadamu
zinapatikana kwa wingi katika Bohari kuu ya dawa MSD kwa masaa 24
zikiwemo dawa za kutibu Malaria, Kifua kikuu, Ukoma ,ARV , dawa za
kutuliza maumivu pamoja na Anti- biotic ili kutimiza na kutekeleza sera
ya mpango wa Afya wa awamu ya tano.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya ,
Maendeleo ya Jamii, Wazee , Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa
mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es salaam
ili kuzungumzia hali ya upatikanaji wa dawa na chanjo nchini.
“Dawa zote muhimu kwa binadamu
zinapatikana kwenye bohari kuu ya dawa kwa masaa 24 kinyume na watu na
Taasisi zisizo za kiserikali kusambaza maneno kuwa MSD imeishiwa dawa
kitendo ambacho sio cha kweli dawa zipo na zinasambazwa kwenye vituo
vyote vya afya” Alisema Mhe. Ummy.
Aidha Ummy amesema kuwa ili
kutekeleza mpango wa sera ya afya ya Serikali ya tano ,jumla ya shilingi
bilioni 251 zimetengwa ili kuweza kuhakikisha dawa za binadamu
zinapatikana kila wakati pindi zinapohitajika kutoka MSD ili kutoa
huduma bora kwa watanzania.
Aliongeza kuwa Serikali imetenga
Bilioni 85 kwa ajili ya kulipa deni linalodaiwa na MSD ili kuhakikisha
Bohari hiyo inajiendesha vizuri na kutokaukiwa dawa pindi zinapohitajika
katika vituo vya afya na kutoa huduma za matibabu kwa muda muafaka kwa
watanzania.
Mbali na hayo Waziri huyo amesema
kuwa tatizo la chanjo kwa sasa limepata ufumbuzi kwani zimeagizwa chanjo
za watoto za kifua kikuu dozi milioni 2, chanjo za Pepopunda dozi
milioni 1.2 na chanjo za Polio ambazo ni dozi 2 ili kuimarisha hali ya
matibabu nchini.
“Tulikuwa na tatizo la chanjo kama
wiki nne zilizopita lakini tumejitahidi na tumeweza kuleta chanjo zote
muhimu pamoja na kuagiza chanjo za surua ambazo zinatarajiwa kuja hivi
karibuni ili kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa wingi nchini”
alisisitiza Waziri huyo.
Aidha amesisitiza kuwa wanahitaji
kununua na kufanya uzalishaji wa dawa katika viwanda vya ndani ili
kuweza kuchangia uchumi wa viwanda vya ndani ili tufikie uchumi wa kati.
Waziri Ummy aliwataka Wakurugenzi
wa Vituo vya Afya pamoja na Waratibu wa Afya wa Wilaya kuagiza dawa MSD
mapema bila ya kusubiri ziishe kabisa kwenye vituo vyao ili kuweza
kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni