Posted byu Esta Malibiche on Oct10.2016 in SIASA
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kimesema hakina mpango wa kufanya mazungumzo au makubaliano na
Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusiana na suala la Uchaguzi uliopita.
Msimamo huo umetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alipokuwa akijibu hoja
zilizotolewa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF Ismail Jussa Ladhu
katika Mahojiano Maalum na Gazeti moja hapa nchini Juzi.
Alisema Uchaguzi umekwisha kazi
iliyokuwepo mbele ya CCM ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama
hicho ya mwaka 2015/2020 ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa katika
kampeni za uchaguzi mkuu na viongozi wa CCM zinatekelezwa kwa vitendo.
Vuai alieleza kwamba kupitia
Mazungumzo na Gazeti la NIPASHE Juma Pili Octobar 9, mwaka huu, Jussa
alinukuliwa akisema CUF inaangalia uwezekano wa kufanya mazungumzo na
CCM kuhusiana na suala la uchaguzi, jambo ambalo CCM haipo tayari kukaa
meza moja na Chama hicho kujadili jambo ambalo lishafanyiwa uamzi halili
kwa mujibu wa kanuzi,taratibu na Sheria za nchi.
Alisema Chama hicho kinaweza
kukikaribisha Chama chochote cha upinzani kufanya mazungumzo juu ya
namna gani ya kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM na
siyo suala la Uchaguzi Mkuu kwani umepita kisheria na serikali
zinaendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Alisema kitendo cha kujadili
serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
sasa ni kwenda kinyume na Sheria za nchini kwani serikali hizo
zimetokana na maamuzi halali ya wananchi kupitia mfumo wa Uchaguzi wa
kidemokrasia.
Aliwataka wafuasi wa Chama hicho
na Wananchi kwa ujumla kupuuza madai yaliyotolewa na Kiongozi huyo hasa
mantiki ya kuundwa kwa serikali ya mpito Zanzibar , hatua ambayo
haiwezekani na inaashiria kuvunja Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.
“CCM hatuna mpango wa kukaa meza
moja na Chama chochote cha upinzani na sio CUF tu, kujadili Uchaguzi
kwani tayari umepita kwa vigezo vyote vya uhalali wa kisheria.
Pia Hoja na Ajenda ya kufanyika
kwa Uchaguzi wa Mpito Zanzibar kwa sasa ni ndoto za mchana ama
kujifurahisha kwa kutafuta umaarufu wa kisiasa usiokuwa na uzani wala
mafanikio kwa wafuasi wa Chama kinachojenga hoja hizo hapa nchini.”,
alisema Vuai na kuongeza kuwa CCM inaamini kwamba Uchaguzi umekwisha na
sasa inajipanga na maandalizi ya Uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alifafanua
kwamba CUF kwa sasa imekosa muelekeo ndiyo maana viongozi wake
wanafikia hatua ya kuwadanganya wafuasi wao kwa mambo ambayo kiuhalisia
wanajua kuwa hayawezekani kufanyika katika historia ya uwanja wa kisiasa
Zanzibar.
Alisema Chama cha kisiasa chochote
pamoja na kuwa na jukumu la kushinda na kusimamisha Dola katika
uchaguzi mkuu bado kinatakiwa kuwa na miongozo imara ya kusimamia
ukweli, haki na uwazi kwa wafuasi na wananchi, vigezo ambavyo
vimekosekana ndani ya CUF toka kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alisisitiza kwamba kazi iliyopo
mbele ya Chama hicho ni pamoja na kujiandaa kwa mambo mbali mbali
yakiwemo Uchaguzi wa ndani wa CCM wa mwaka 2017, kwa ajili ya kupata
viongozi makini na mahodari ambao pia watakuwa na jukumu la kusimamia
maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Alilitaja jukumu la msingi
linalotekelezwa na chama hicho ni pamoja na uhakiki wa Mali za CCM ili
kujiridhisha zaidi ikiwa ni mkakati wa uimarishaji hali ya siasa na
uchumi ndani ya CCM.
Aliwasihi wafuasi wa Chama hicho
na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu na kushirikiana
kikamilifu na serikali zote mbili Serikali ya Awamu ya saba ya Mapinduzi
ya Zanzibar na Serikali ya awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania .
Aidha aliwataka wananchi kuwafichua baadhi ya wanasiasa wanaojihusisha na vitendo vya kuharibu amani na utulivu wa nchi.
0 maoni:
Chapisha Maoni