Ijumaa, 28 Oktoba 2016

OLE MEDEYE: MUSWADA WA HABARI UMEKUSUDIA KUBORESHA MASLAHI YA WANAHABARI

Posted by Esta Malibiche on Oct 28.2016 in NEWS

indexNa Ismail Ngayonga-MAELEZO-Dar es Salaam
WADAU wa habari nchini wametakiwa kuzingatia maslahi ya taifa na tansia ya habari kwa mapana zaidi kuhusu muswada wa sheria ya huduma za habari wa mwaka 2016, kwa kuwa muswada huo umekusudia kuboresha maslahi yao.
Hayo yamesemmwa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha UDP, Goodluck Ole Medeye katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi wakati akitoa msimamo wake kuhusu maudhui ya muswada huo.
Medeye alisema muswada huo umekuja katika wakati mwafaka ikiwemo muswada umekusudia kuanzishwa kwa vyombo maalum vya kusimamia tasnia ya habari ikiwemo vyombo vya maadili, maslahi, haki, na usalama wa waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Medeye alisema muswada huo hauna budi kuungwa mkono na wadau kwa kuwa umelenga kuboresha maslahi ya wanahabari ikiwemo sharti la kisheria la kuwataka wamiliki wa vyombo vya habari kuwakatia bima ya afya na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Aidha Medeye alisema muswada huo ni vyema ukaongeza kipengele cha kuwataka wamiliki kuajiri waandishi wa kudumu katika vyombo vya habari, kwani wengi wa waandishi waliopo katika tasnia hiyo ni wawakilishi pekee, ambao mmiliki hawajibiki nae.
“Uhuru wa kweli katika tasnia ya habari utapatikana pale ambapo, maslahi yao yataboreshwa ikiwemo suala zima la utoaji wa bima na maslahi mengine, ambayo katika muswada huu yamewekwa wazi zaidi” alisema Medeye.
Aidha Medeye alisema kupitishwa kwa muswada huo kutaiwezesha fani ya habari kuendelea kuheshimika na kuaminika zaidi kama zilivyo fani za udaktari, uuguzi, sheria na kadhalika.

0 maoni:

Chapisha Maoni