Alhamisi, 13 Oktoba 2016

SERIKALI YA TANZANIA IMEPOKEA Tsh BILIONI 97 TOKA CHINA

Posted by Esta Malibiche on Oct13.2016 in NEWS

fed2

Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage (kushoto) na Naibu Waziri wa Biashara wa Serikali ya China Dkt. Qian Keming (kulia), wakibadilishana hati ya makubaliano ya Kikao cha Tano cha Kamati ya pamoja ya Ushirikiano wa masuala ya Uchumi, Ufundi na Biashara Baina Serikali ya Tanzania na China, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es salaam.
fed1
Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage (wa pili kushoto) na Naibu Waziri wa Biashara wa Serikali ya China Dkt. Qian Keming (wa pili kulia), wakisaini Makubaliano ya Kikao cha Tano cha Kamati ya pamoja ya Ushirikiano wa masuala ya Uchumi, Ufundi na Biashara Baina Serikali ya Tanzania na China, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es salaam.


fed3
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Dorothy Mwanyika (wa pili kushoto) na Naibu Waziri Biashara wa Serikali ya China Dkt. Qian Keming (wa pili kulia), wakisaini Mkataba wa Ushirikiano wa masuala ya Uchumi na Ufundi baina ya Serikali ya Tanzania na China, katika ukumbi wa Wizara jijini Dar es salaam.
fed4
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Dorothy Mwanyika (kushoto) na Naibu Waziri Biashara wa Serikali ya China Dkt. Qian Keming (kulia), wakibadilishana Mkataba wa Ushirikiano wa masuala ya Uchumi na Ufundi baina Serikali ya Tanzania na China, katika ukumbi wa Wizara jijini Dar es salaam.
fed5
Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu masuala ya kibiashara na Ufundi baada ya kusaini Makubaliano ya Kikao cha Tano cha Kamati ya pamoja ya Ushirikiano wa masuala ya Uchumi, Ufundi na Biashara Baina Serikali ya Tanzania na China, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es salaam.
…………………………………………………….
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano ya kikao cha tano cha kamati ya pamoja ya ushirikiano wa masuala ya uchumi, ufundi na biashara kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China.
Katika makubaliano hayo Serikali ya Tanzania imepokea kiasi cha shilingi Billioni 97 za kitanzania ambao utafadhiliwa na Serikali ya China kwa ajili ya kusaidia sekta ya Elimu, Afya na Usalama kwenye viwanja vya ndege na Bandari nchini.
Makubaliano hayo yamefanyika  leo jijini Dar es salaam katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Fedha na Mipango na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, pamoja na Naibu Waziri wa Biashara wa China Qian Keming.
Waziri Mwijage alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kusaidia Serikali ya Tanzania kuboresha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta ya Elimu, Afya, na Usalama wa Bandari na Viwanja vya Ndege ili kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na China uliodumu kwa muda mrefu.
Aidha, Waziri Mwijage alisema kuwa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya China imekubaliana kushirikiana katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo Serikali ya China imeahidi kutekeleza Mradi wa Mlandizi wa utengenezaji wa chuma unaotarajia kuanza wakati wowote.
Pia alisema kuwa, Serikali ya China imeahidi kujenga kiwanda cha Vigae katika eneo la Mkuranga ambacho kitakuwa na uwezo wa kutengeneza kilomita za mraba 80,000 kwa siku ambapo uzalishaji  huo utaanza mara baada ya kukamilika kwa bomba la gesi kutoka Mtwara na kinatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu.
Vilevile alisema kuwa ifikapo mwaka 2019 Tanzania itaachana na uvaaji wa nguo za mitumba, hivyo Serikali ya China imeahidi ujenzi wa kiwanda cha nguo nchini chenye uwezo wa kuajiri wafanyakazi 14,000 na kuzalisha nguo baada ya kukamilisha upatikanaji wa ekari 700 za eneo.
Naye Naibu Waziri wa Biashara wa China Qian Keming alisema kuwa Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali kwani imeshuhudia mabadiliko katika sekta ya miundombinu, viwanda na biashara.
Pia Qian Keming, amewakaribisha Watanzania kuhudhuria maonesho mbalimbali yanayofanyika nchini China kama wao wanavyoshiriki maonesho mbalimbali ya nchini Tanzania.
Katika hatua nyingine Serikali ya Tanzania na China imesaini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi ambao utaiwezesha Serikali ya Tanzania kuimarika katika masuala ya uchumi.
Mkataba huo umesainiwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dorothy Mwanyika na Naibu Waziri wa Biashara wa China Qian Keming unaolenga kuboresha mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo.
Mbali na hayo Serikali ya Tanzania na China imekuwa na majadiliano yaliohusu uboreshaji wa Bandari ya Bagamoyo na maeneo yake kibiashara, nia ya kujenga Reli ya kati “Standard Gauge”, Reli ya Tazara, Bandari ya Zanzibar, pamoja na Kiwanja cha ndege Zanzibar.

0 maoni:

Chapisha Maoni