Ijumaa, 28 Oktoba 2016

Mafunzo ya Wajumbe wa Kamati ya Shule ya Msingi Uhelela Yapunguza Idadi ya Wanafunzi Watoro

Posted by Esta Malibiche on Oct 28.2016 in NEWS

imagesNa. Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-T) imefanikiwa kupunguza utoro katika Shule ya Msingi Uhelela iliyoko Wilayani Bahi mkoani Dodoma kupitia mafunzo ya usimamizi wa shule  wanayopewa wajumbe wa Kamati za Shule za Msingi Mkoani humo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo Isaya Chimela aliyasema hayo, Wilayani Bahi  wakati wa mahojiano na timu ya Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Wilaya hiyo .
“Utoro wa wanafunzi hapa shuleni kwetu umepungua baada ya sisi wajumbe wa Kamati ya Shule kupatiwa mafunzo ya usimamizi wa shule kupitia EQUIP-T . Pia, tumeweka zamu za wajumbe kufuatilia mahudhurio ya wanafunzi shuleni mara mbili kwa wiki, ” alifafanua Chimela.
Aidha aliendelea kwa kusema kuwa ufuatiliaji wa karibu wa mahudhurio kwa wanafunzi wa shule hiyo ndiyo uliyopelekea kupungua kwa  kiwango cha utoro kwa wanafunzi hao.
Vile vile Kamati hiyo imekuwa ikiwaelimisha wazazi ambao watoto wao ni watoro, juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wao na namna ambavyo watoto hao watafanikiwa ikiwa watapata elimu.
Kutokana na elimu hiyo wazazi wamekuwa wakishirikiana na Kamati hiyo katika kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya taaluma ya watoto wao.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Dankan Kamwela amesema kuwa shule hiyo imefanikiwa kupunguza utoro kutoka wanafunzi 127 (30%) kwa siku mwaka 2015 hadi wanafunzi 12 (8%) kwa siku mwaka 2016.

0 maoni:

Chapisha Maoni