Posted by Esta Malibiche on Oct 31.2016 in NEWS
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akipata maelezo
kutoka kwa Bw. Leonard Kushoka wa pili kulia katika hatua mbalimbali za
uzalishaji wa nishati mbadala.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akiangalia mkaa
uliokamilika baada ya uzalishaji, mkaa ambao ni rafiki kwa mazingira.
………………
Na Lulu Mussa TABORA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. Jauary
Makamba amempongeza Bw. Leordard Kushoka kwa kubuni kiwanda
kinachotengeza nishati mbadala rafiki kwa mazingira.
Akiwa Mkoani Tabora, Waziri
Makamba alipata fursa ya kutembelea kiwanda hicho na kusema kuwa
Serikali inathamini sana ubunifu na uvumbuzi hasa unao okoa mazingira.
“Bwana Kushoka mimi nakupongeza sana, niliona jitihada zako kupitia
kipindi cha televisheni na kuamua kukuita na kukusaidia” alisisitiza
Waziri Makamba.
Katika kuthamini mchango wa
Kiwanda hicho cha “Kuja na Kushoka” Ofisi ya Makamu wa Rais imemsaidia
Bw. Kushoka kupata haki miliki ya Kiwanda hicho.
Awali Bw. Leonard Kushoka,
Mkurugenzi wa Kuja na Kushoka Tools Manufacture Group amesema kuwa
kiwanda chake kimefanikiwa kutoa ajira kwa vijana 13 na kufanikiwa
kubuni teknolojia mbalimbali rafiki kwa mazingira ambapo mpaka sasa
wamefanikiwa kuwafikia vijana zaidi ya 50 katika Wilaya za Tabora
Manispaa, Urambo, Kaliua, Mlele pia Katavi na kufanikiwa kuwafundisha
utengenezaji wa Majiko banifu yanayopunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa
asilimia 50.
Pia Kiwanda hicho kimefanikiwa
kubuni mashine ambayo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha kilo 160 kwa saa kwa
kutumia dizeli lita 5 na kuzalisha wastani wa Kilo 1000 za mkaa mbadala
na pia Kiwanda hicho kimefanikiwa kubuni mtambo kwa kukaushia tumbaku
kwa kutumia taka kavu au mabaki yote ya mazao kama maganda ya karanga,
randa za mbao, magunzi ya mahindi na masuke ya mpunga.
Bw. Kushoka amesema kuwa “Mtambo
huu umetoa matokeo mazuri katika ukaushaji wa tumbaku kwani wastani wa
matumizi ya taka kilo 3 hukausha kilo moja ya tumbaku kwa kutumia mabani
ya kisasa”
Bw. Kushoka amemuomba Waziri
kuisaidia Kampuni hiyo kupata mafunzo mbalimbali ya namna bora zaidi ya
kubuni na kuendeleza uzalishaji wa nishati mbadala hasa katika nchi
zinazofanya vizuri zaidi.
‘Kuja na Kushoka” ilianzishwa rasmi mwaka 2000 na kupata usajili mwaka 2013 na kupewa hati (TMC/CO/CBO/48).
Waziri Makamba akiwa katika Mkoa
wa Tabora pia amepata fursa ya kutembelea Wilaya ya Nzega na Igunga,
akihitimisha ziara yake ya Mikoa 10 hapa nchini yenye changamoto za
kimazingira.
0 maoni:
Chapisha Maoni