Ubalozi
wa China nchini umeipatia Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo
vifaa vya ofisi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 ikiwa ni
kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Serikali hizo mbili.
Hatua
hiyo imekuja ikiwa na lengo la kusaidia katika kukuza na kuendeleza
sekta ya sanaa ambayo katika mpango wa miaka mitano ya maendeleo ya
Serikiali inatakiwa kuongeza ajira pamoja na pato la taifa kupitia kazi
mbalimbali za sanaa.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo Jijini Dar es Salaam Kaimu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw. Petro Lyatuu
aliushukuru Ubalozi huo kwa mchango wao wa kuhakikisha sekta ya sanaa
inakuwa na kuleta mabadiliko nchini.
“Tunashukuru
Ubalozi wa China kwa kutupatia vifaa hivi ambavyo vitasaidia sana
utendaji katika Sekta ya Sanaa ambayo inaendelea kukua kwa kasi hapa
chini na kusaidia kuimarisha ushirikiano mzuri baina ya Serikali yetu na
China”Alisema Bw. Petro Lyatuu.
Naye
Mshauri wa masuala ya Utamaduni kutoka Ubalozi huo Bw Gao Wei amesema
kwamba China itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara katika kuendeleza
Sanaa kwa kutoa misaada mbalimbali kwa kadri itakavyohitajika.
“Tutaendelea
na ushirikiano huu sio tu kwa kutoa msaada wa vifaa bali pia
kubadilishana uzoefu na taaluma ya Sanaa ili Sekta hii ikue na
kuheshimika na kutambulika rasmi kama ajira ”Alisema Bw Gao.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bibi Leah
Kihimbi amesema kuwa vifaa hivyo vitaimarisha utendaji kazi wa Sekta ya
Sanaa ukizingatia kuwa ni Sekta ambayo imebeba dhamana kubwa ya
kutangaza Sanaa ndani na nje ya nchi.
Vifaa
vilivyotolewa na Ubalozi wa China ni pamoja na Komputa 4,Komputa
Mpakato 1,Kamera ya video moja na Luninga vyote vikiwa na jumla ya
dhamani zaidi ya milioni 20.
0 maoni:
Chapisha Maoni