Posted by Esta Malibiche on Oct12.2016 in NEWS
Mkuu wa Chuo cha Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila.
Na May Simba-MAELEZO
Wanazuoni nchini wanatarajia
kukutana na kuchambua miiko na maadili ya viongozi wa Umma tarehe 14,
Octoba mwaka huu kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 8: 00 mchana, katika
ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere (MNMA), ili kuenzi
siku ya kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha
Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila alipokuwa akiongea na
waandishi wa habari leo, Jijini Dar es Salaam kuhusu kongamano la
kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Profesa Mwakalila amesema kuwa
Chuo hicho kimeandaa Kongamano hilo ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Baba wa
Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliamini kuwa kila nchi
Duniani ina miiko yake na maadili inayowaongoza viongozi wa Umma.
“Chuo kimewaalika wanazuoni watano
ambao ni Dkt Harun Kondo atakaye chambua Azimio la Arusha, aliyekuwa
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mkama na Mzee Joseph Butiku watachambua Miiko
ya uongozi pamoja na Ibrahim Kaduma na Mhe Philip Mangula watakaojadili
maadili ya viongozi,” alisema Prof. Mwakalila.
Mbali na hayo Prof. Mwakalila
amesema kuwa Miiko ya uongozi na maadili ya viongozi wa Umma
ilisisitizwa na Mwalimu mara baada ya Uhuru na baadaye kusisitizwa zaidi
katika Azimio la Arusha la mwaka 1967.
Vile vile Mwalimu Nyerere katika
hotuba zake alikuwa akiwaasa viongozi wa Umma kuwa na maadili na kufuata
miiko ya Uongozi ili kuwa mfano bora kwa jamii inayowazunguka.
Kongamano hilo linafanyika ikiwa
ni maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa
ambapo kauli mbiu ya kongamano hilo ni “Miiko ya uongozi na Azimio la
Arusha”.
0 maoni:
Chapisha Maoni