KATIBU
Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Elisante
Ole Gabriel anatarajiwa kufungua kongamano kuhusu mabadiliko ya mifumo
ya uendeshaji katika klabu za soka nchini.
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Jumamosi Oktoba 22, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuhusu
mifumo ya kiuendeshaji ambayo klabu kongwe nchini za Simba na Yanga
zipo mbioni kuingia na limeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA).
Kongamano
hilo litaanza saa nne na nusu asubuhi na litarushwa live (mubashara) na
kituo cha televisheni cha Azam kupitia chaneli yake ya Azam Two.
Dhamira
kubwa ya kongamano hilo ni kupata maoni ya kitaalamu kuhusu mifumo
hiyo, ambapo Simba ipo mbioni kuingia mambo ya hisa, wakati Yanga
utaratibu wa kukodishwa.
Baadhi
ya mambo yatakayojadiliwa ni namna ya kuendesha klabu za soka
kibiashara, uwekezaji, mambo ya hisa na masuala ya uthamini kukiwa na
watalaamu kutoka taasisi mbalimbali nchini.
Pia
kutazungumzwa umuhimu wa mabadiliko katika klabu hizo na harakati za
kuzibadili zilivyoanza miaka ya nyuma na matokeo yake yalivyokuwa.
Lengo
ni kujadili kitaalamu bila ushabiki wa namna yoyote kwani nia ni
kujenga na kuimarisha soka na michezo kwa ujumla hapa nchini na ndiyo
sababu tumealika wataalamu wa kada mbalimbali, viongozi wa zamani wa
soka kwa tofauti na baadhi ya wadau wa soka.
Nawasilisha,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
21/10/2016
0 maoni:
Chapisha Maoni