Posted by Esta Malibiche on Oct 28.2016 in NEWS
Na Jovina Bujulu MAELEZO- Dar es Salaam
IMEELEZWA kuwa kuanzishwa kwa
mfuko wa mafunzo wa habari uliopo katika muswada wa sheria ya huduma
za habari utasaidia kuibua weledi, stadi, ujuzi, na ubobeaji kwa
waandishi wa habari katika utelekezaji majukumu yao ya kila siku.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Dkt. Samwilu
Mwaffisi wakati alipokuwa akizungumzia kuhusu maudhui yaliyopo katika
muswada wa huduma za habari.
“Naunga mkono uanzishwaji wa mfuko
wa mafunzo ya wanahabari kwa asilimia 100 isipokuwa mafunzo hayo
yajikite katika mafunzo ya vitendo zaidi kuliko nadharia, kwani vyuo
vingi tulivyonavyo nchini vinafundisha zaidi nadharia” alisema Dkt.
Mwaffisi.
Akifafanua zaidi alisema kanuni
zitapotungwa katika uendeshaji wa mfuko huo mkazo wake uelekezwe katika
mafunzo zaidi, ambapo wanahabari wanaosomea shahada mafunzoyao yaanze
mwaka wa kwanza wa masomo yao na baada ya kuhitimu shahada ianzishwe
sheria ya kusoma kwa vitendo kwa kipindi fulani.
Aidha Dkt. Mwaffisi alisema kuwa
ni vyema mfuko wa mafunzo ukawajengea uwezo wanahabari katika ubobezi wa
fani tofauti tofauti na hivyo kuwapa uzoefu wa kuandika fani kwa weledi
zaidi.
Akizungumzia kuhusu Bodi ya
ithibati inayothibitisha wanahabari, Dkt. Mwaffisi alisema jambo hilo
limekuja wakati mwafaka kwani itamfanya mwandishi awajibike kwa jamii.
“Uthibitishwaji wa wanahabari
utawafanya waandike kwa weledi na ufanisi zaidi wakizingatia maadili ya
taaluma na jamii ili kuepuka adhabu ambayo wanaweza kupewa na bodi ya
ithibati iwapo watavunja maadili” aliongeza Dkt. Mwaffisi.
0 maoni:
Chapisha Maoni